Atwoli akemea FKE kwa kupinga ushuru wa ujenzi wa nyumba
COLLINS OMULO na CHARLES WASONGA
KATIBU Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU), Francis Atwoli, ameshambulia Shirikisho la Waajiri Nchini (FKE) kwa kupinga mpango wa serikali wa kutoza wafanyakazi na waajiri ushuru wa asilimia 1.5 kufadhili hazina ya ujenzi nyumba za gharama nafuu.
Bw Atwoli alisema muungano huo unaunga mkono ushuru huo mradi serikali ikubali pendekezo lao la kutaka waongezwe mishahara kwa kima cha asilimia 15.
“Nawaambia kuwa huu ushuru wa nyumba ni mzuri. Huu ni mpango mzuri kwani utawafaidi wafanyakazi. Niliambia serikali kwamba ili tukubali mpango huo, watupe nyongeza ya mishahara ya asilimia 15,” akasema jana alipokutana na wakuu wa wafanyakazi katika makao makuu ya COTU, Gikomba, Nairobi.
Bw Atwoli alidai kuwa Mkurugenzi Mkuu wa FKE Jacquiline Mugo anapinga utekelezaji wa ushuru huo kama njia ya kuonyesha chuki kwa COTU baada ya muungano huo kujitahidi kuhakikisha nyongeza ya mishahara ya asilimia 5 iliyoahidiwa na serikali imechapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.
“Bi Mugo sasa anajifanya kwamba anawatetea kwa kupinga ushuru wa hazina ya nyumba. Hii kesi ilikuwa ni yetu. Anasema kuwa kesi hiyo ilikuwa ikiendeleza masilahi ya umma na kwamba, mimi siwakilishi masilahi ya umma. Nitamshinda jinsi ambayo nimekuwa nikimshinda kila mara,” alisema.
Kauli ya Bw Atwoli inaonyesha kuwa COTU sasa imebadili msimamo wake kuhusu ushuru huo wa nyumba ilhali mwaka jana ilidai unakiuka katiba kwa sababu wafanyakazi na waajiri hawakushauriwa kuhusu kuanzishwa kwake.
“Tuko na jumla ya wafanyakazi 2.5 milioni walioajiriwa katika sekta ya umma na kibinafsi ambao wanapangiwa kuchangia hazina hiyo na serikali inalenga kujenga nyumba milioni moja katika kipindi cha miaka minne ijayo. Ni vigezo vipi vitatumika kuwagawanya nyumbani hizo?” Bw Atwoli aliuliza Septemba mwaka jana.
Ushuru huo wa nyumba ulioanzishwa na serikali kupitia Mswada wa Fedha wa 2018 ambao ulitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kupitishwa na wabunge katika katika mazingira ya rabsha bungeni.
Chini ya mpango huo, serikali itataka asilimia 1.5 ya mshahara wa kila mfanyakazi huku kiasi sawa na hicho kikichangiwa pia na mwajiri. Hii ina maana kuwa wafanyakazi wanaopokea Sh166,000 na zaidi kila mwezi watachangia kiasi kisichozidi Sh2,500 kila mwezi kwa hazina hiyo.
Mpango wa serikali wa kutekeleza utozaji huo ulipata pigo Ijumaa baada ya mahakama kuu kukataa kuondolewa kwa kesi inayopinga utekelezaji wa mpango huo.
Mahakama ya Juu ilikataa kuruhusu makubaliano kati ya Cotu na serikali kwamba, kesi hiyo iondolewe baada ya washika dau wengine kuibua pingamizi.
Wahusika hao, wakiwemo FKE na Shirikisho la Watumiaji Bidhaa (COFEK) wote walikuwa wamewasilisha ombi wakitaka wajumuishwe katika kesi hiyo iliyowasilishwa na Cotu.
Viongozi wa mashirikisho hayo walisema hawakuwa wameshauriana kabla ya Cotu kukubaliana na serikali. Walikatalia mbali makubaliano hayo wakisema hawakuwa na nia ya kuondoa kesi hiyo.
Stakabadhi hiyo ya makubaliano ilisema kuwa Cotu, FKE na Cofek zilikubaliana na wizara ya uchukuzi na miundo msingi kuondoa kesi hiyo inayopinga utekelezaji wa ushuru wa nyumba.