• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Baadhi ya vifaa vya kujikinga corona vina dosari – Kagwe

Baadhi ya vifaa vya kujikinga corona vina dosari – Kagwe

Na BENSON MATHEKA

WAZIRI wa Afya, Mutahi Kagwe, amekiri kwamba baadhi ya vifaa vya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya virusi vya corona wakiwa kazini vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi viligunduliwa kuwa na dosari na kupigwa marufuku.

Bw Kagwe alisema shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini halikuidhinisha vifaa hivyo kwa sababu vilikuwa hatari kwa afya ya wahudumu hao.

“Kwa sasa, tumeamua kutumia vifaa vinavyotengenezewa nchini kwa sababu ubora wake umeidhinishwa na madaktari. Hatukukubali kuweka hatarini maisha ya madaktari wetu ambao wanafanya na wanaendelea kufanya kazi nzuri,” Bw Kagwe alisema.

Alisema kampuni za humu nchini zina uwezo wa kutengeneza vifaa bora zaidi.

Bw Kagwe aliwataka Wakenya kutembelea vituo vya afya kutibiwa wanapougua akisema huduma zinaendelea kama kawaida.

“Tunawahimiza watu kutafuta huduma za matibabu kwa sababu hospitali zetu zimeweka mikakati ya kuzuia maambukizi ya corona kwa wanaotafuta matibabu ya maradhi mengine,” alisema.

Bw Kagwe alisema hayo huku idadi ya watu walioambukizwa corona nchini ikifika 1,161 baada ya watu 52 zaidi kuthibitishwa kuwa na virusi hivyo huku Nairobi ikiwa na visa 23. Visa saba vilithibitishwa katika Kaunti ya Mombasa na Busia ikawa na idadi sawa.

Miongoni mwa visa 23 vilivyothibitishwa katika Kaunti ya Nairobi, saba vilikuwa mtaa wa mabanda wa Kibra.

“Hali katika mtaa wa Kibra inatia wasiwasi na tutachukua hatua kali zaidi. Wataalamu wetu wamo humo wakitathmini hali na uamuzi tutakaochukua utategemea ushauri wa kisayansi watakaotupatia,” alisema Bw Kagwe.

Akizungumza akiwa kaunti ya Machakos kutathmini maandalizi ya serikali za kaunti katika kupigana na janga hilo, Bw Kagwe alisema ushirikiano wa viwango vyote vya serikali ni muhimu katika vita dhidi ya corona.

Bw Kagwe alisema Kenya haitaruhusu dawa ya mitishamba kutoka Madagascar inayodaiwa kuponya virusi vya corona.

Alisema dawa hiyo haijafanyiwa utafiti na kuidhinishwa na wataalamu.

“Hatuwezi kufanya majaribio na maisha ya Wakenya,” alisema.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua alisema madereva wa malori ya mizigo hawataruhusiwa kupitia kaunti hiyo wakithibitisha hawajapimwa virusi vya corona.

“Ili kulinda watu wetu, hakuna dereva wa lori la kubeba mizigo atakayeruhusiwa kaunti ya Machakos bila cheti cha kuthibitisha hana virusi vya corona,” alisema Dkt Mutua.

Alisema kwamba madereva hao watakuwa wakikaguliwa katika mipaka ya kaunti hiyo.

Wakati huo huo, Dkt Mutua aliondoa marufuku ya kusambaza pombe katika Kaunti ya Machakos lakini akasema shughuli hiyo inafaa kufanywa kwa kuzingatia kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona.

You can share this post!

KAMAU: Imani za kidini zisiwe kikwazo kwenye vita dhidi ya...

Uhuru azidi kumkalia Ruto

adminleo