Bandari yetu haitatwaliwa, tutakopa zaidi kutoka Uchina – Uhuru
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amekana madai kuwa Bandari ya Mombasa ilitumiwa kama dhamana kwa mkopo kutoka kwa Benki ya Exim na hivyo kuwa katika hatari ya kutwaliwa na China endapo Kenya itashindwa kulipa deni hili.
Alisema Kenya itaendelea kukopa pesa kutoka China na mataifa mengine ulimwenguni licha ya wakosoaji kudai kuwa haitamudu kulipa madeni yake ambayo yametimu Sh5.1 trilioni.
“Bandari yetu iko salama. Yale mnayosikia ni uvumi tu ambayo hayana ukweli wowote. Mlisikia China pia ikikana madai hayo ….na mkitaka stakabadhi za mkataba kati yetu na China kuhusu mkopo huo nitawapa kesho,” Rais Kenyatta akasema kwenye mahojiano na wanahabari katika Ikulu ya Mombasa Ijumaa usiku.
“Nitaendelea kukupa ili kuendeleza taifa hili. Mikopo ni muhimu kwa taifa lolote ambalo linalenga kuimarisha miundo msingi yake,” akaongeza huku akifafanua kuwa Kenya imekuwa ikilipa mikopo yake kwa wakati.
Mapema mwezi huu ripoti moja kutoka Afisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Edward Ouko ilidai kuwa mnamo 2013 Kenya ilitumia Bandari ya Mombasa kama dhamana kwa mkopo wa Sh327 bilioni zilizotumiwa kujenga awamu ya kwanza ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi.
Hii ina maana kuwa endapo Kenya itafeli au ichelewe kulipa mkopo huo basi China itakuwa huru kutwaa usimamizi wa bandari hiyo ili kujesha pesa zake. Bandari hiyo huzalisha Sh42.7 bilioni kwa wastani, kila mwaka.
Mnamo Desemba 25, msemaji wa Wizara ya Masuala ya Kigeni ya China Hua Chunying alipuuzilia mbali hofu kwamba bandari hiyo iko katika hatari ya kutwaliwa na China endapo Kenya itashindwa kulipa mkopo wa Sh327 bilioni.
“Tumefanya uchunguzi katika asasi husika za kifedha za China na kubaini kuwa madai kwamba Kenya ilitumia bandari ya Mombasa kama dhamana katika makubaliano yake, na Benki ya Exim, ya ulipaji mkopo, ni uwongo,” Bw Chunying akasema kwenye taarifa.
Hata hivyo, msemaji huyo hakufichua mali ambayo Kenya ilitumia kama dhamana kwa mkopo huo wa ujenzi wa reli ya kisasa.
Vile vile, Rais Kenyatta, mnamo Ijumaa, alifeli kuwafichua wanahabari aina ya dhamana hiyo ambayo sio Bandari ya Mombasa ikizingatiwa kuwa mkopo mkubwa kiasi hicho huhitaji kuwekewa dhamana.
Kiongozi wa taifa alisema Kenya inashirikiana na mataifa washirika ambayo yanaelewa mahitaji yake kimaendeleo, China ikiwa ni moja yao.
“China na mshirika mkuu wa Kenya kimaendeleo jinsi ilivyo Benki ya Dunia na mataifa kama Japan, Ufaransa na Ujerumani,” Rais Kenyatta akaeleza.