Habari MsetoMakala

BODABODA: Kizingiti kikuu cha hali ya usalama nchini

March 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

CHARLES WASONGA na TITUS OMINDE

PIKIpiki za uchukuzi wa abiria, maarufu, boda boda, hupendwa na watu wengi nchini kutokana na kutokana na unafuu wake pamoja na uwezo wa kupenya mitaani na vijijini ambako magari ya uchukuzi wa umma hayawezi kufika.

Hii ndio maana sekta hii ya uchukuzi imekuwa kwa kasi katika miaka ya hivi karibu ambapo mwaka jana wahudumu wa bodaboda waliweza kuchuma mapato ya kima cha Sh219 bilioni kulingana na takwimu kutoka muungano wa Motor Assemblers Association of Kenya (MAAK).

Lakini licha ya kiwango hiki cha faida, bodaboda hizi zimekuwa zikitumika kama vyombo vya kurahisisha utekelezaji wa uhalifu katika maeneo ya mijini na mashambani.

Msemaji wa polisi Charles Owino anasema siku hizi kati ya visa kumi vya wizi katika maeneo ya mijini, sita hutekelezwa na wahalifu wanaosafiri kwa piki piki hizo wakijifanya wahudumu wa bodaboda.

“Wahalifu hupenda kutumia pikipiki ili waweze kukwepa maafisa wa polisi katika barabara za miji zenye misongamano ya magari pamoja na vichochoroni katika mitaa na vijiji. Magari ya polisi hukabiliwa na wakati mgumu wanapowaandama wahalifu wanaotumia pikipiki,” anasema.

 

Uhalifu

“Isitoshe, uchunguzi wetu umebaini kuwa huenda baadhi ya waendesha boda boda hushirikiana na walihalifu ambao huwahangaisha wakazi katika miji mikuu nchini, haswa Nairobi, Mombasa, Eldoret, Kisumu na Nakuru,” Bw Owino anaongeza.

Lakini wahudumu wa boda boda wanajibu kwa kusema kuwa sio wote huhusika katika visa vya uhalifu.

“Japo kuna wachache miongoni mwetu ambao ni watundu na ambao hushirikiana na wahalifu lakini hiyo sio sababu ya kuwahudumu wote hapa Nairobi na kote nchini,’ mwenyekiti wa Muungano wa Wanabodaboda Kaunti ya Nairobi Charles Gichira alinukuliwa akisema.

“Sio sahihi kudai kuwa wahudumu wote wa bodaboda hushiriki uhalifu. Tuko tayari kuketi na serikali ya kaunti ya Nairobi na idara ya polisi kukabiliana na wachache miongoni mwetu ambao hudaiwa kushirikiana na wahalifu,” akasema, akirejelea hatua ya serikali ya kaunti ya Nairobi kuwapiga marufuku wanahudumu hao katikati mwa jiji kwa kuendeleza uhalifu.

Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi katika kaunti ya Nairobi Peter Mbaya anasema maafisa wake wataendelea kukishirikiana na polisi kuendesha operesheni ya kuwaondoa bodaboda na wachuuzi katikati wa jiji katika harakati za kuimarisha usalama.

“Tunashawishika kuwa baadhi ya bodaboda hawa ndio hutumika kufanikisha wizi na aina zingine za uhalifu katikati haswa katikati mwa jijini. Kwa hivyo, operesheni ya kuwaondoa wahudumu hawa na wachuuzi itaendelezwa bila hadi tuhakikishe jiji hili ni salama,” anasema akiongeza kuwa kufikia sasa zaidi ya pikipiki 30 zimenaswa katika operesheni hiyo kwa jina “Operation Fagia Nairobi County”.

Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Central Bw Robinson Thuku anasema baadhi pikipiki ambazo hutumika katika uhalifu huwa zinafafana na zile ambazo hutumika kuwasafirisha abiria.

Mwanabodaboda huyu amekiuka sheria za trafiki kwa kubeba abiria watano. Picha/ Hisani

Kisiki kikuu

“Bodaboda hawa, japo sio wote, wamegeuka kuwa kizingiti kikuu kwa juhudi zetu za kudhibiti usalama haswa katikati mwa jiji. Wahalifu huwatumia kutoroka baada ya kuwaibia wafanyabishara na hata wapita njia. Sharti waondolewe kabisa,” afisa huyo alisema majuzi.

Mbunge wa Starehe Bw Charles Njagua Kanyi amepinga hatua hiyo akisema ilitolewa pasina wadau wote kushauriwa.

“Sio haki kwa serikali ya kaunti ya Nairobi na polisi kuwafurusha wanabodaboda kutokana kisingizio kuwa wao hushirikiana na wahalifu ilhali hakuna mashauriano yoyote yaliyofanywa na wahusika,” akasema mbunge huyo ambaye aliwasilisha kesi mahakama kupinga marufuku hiyo.

Katika kaunti za pwani visa kadhaa vimeripotiwa ambapo wahalifu, wenye silaha, wamekuwa wakiwashambulia watu mchana peupe na kuwapora, kisha kutoroka kwa pikipiki za bodaboda.

Kulingana na ripoti ya polisi visa hivyo vimekithiri mno katika miji ya kitalii ya Mombasa na Malindi. Na polisi wamechukua hatua kwa kuanzisha msako mkali dhidi ya wahudumu wa pikipiki hizo wengi wao wakipatikana bila leseni ya kuhudumu.

Mnamo Januari mwaka huu, watu watatu ambao walikuwa na bunduki aina ya AK47 waliwapiga risasi na kuwaua wazee wawili katika eneo la Mwembe Kuku. Wahasiriwa hao, Mohamed Shaibu na Mohamed Sharifuddin ni wakazi wa eneo hilo.

Wahudumu wa boda boda pia wamekuwa wakichukua sheria mikono mwao kwa kuwaharibu magari yahapohusika katika ajali na mmoja wao.

 

Kuchoma mabasi

Kwa mfano mapema mwaka huu walichoma basi la kampuni ya Simba Coach katika eneo la Msabaha, Malindi. Hii ni baada ya basi hili kugongwa mwanabodaboda mmoja na kumuua katika barabara ya Malindi –Mombasa.

Na mnamo Desemba 2017 wahudumu hao katika kaunti ya Homa Bay walichoma basi jingine la abiria lilihusika katika ajali na mmoja wao. Basi hilo la kampuni ya Otange lilikuwa limeshusha abiria mjini Homa Bay ndipo mwanabodaboda akaligonga kutoka nyuma na akajeruhiwa.

Wenzake walifika mahala hapo kwa wingi na kulitekeleza basi hilo. Zaidi ya abiria 20 waliokuwa ndani ya basi hilo walitoroka kupitia madirisha kuokoa maisha yao.

Walinda usalama mjini Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu pia wanakabiliwa na kibarua kigumu kukabiliana na ongezeko la visa vya uhalifu vinavyohusisha piki piki za boda boda.

Wamelazimika kupiga marufuku uchukuzi wa bodaboda nyakati za usiku kama njia moja ya kudumisha usalama.
Kamishna wa kaunti ya Uasin Gishu Bw Abdi Hassan alisema marufuku hiyo ilianza kutumika mwaka mmoja uliopita kama mojawapo ya mkakati wa

kudhibiti visa vya utovu wa usalama usafiri katika mji huo wenye shughuli nyingi.

 

Usiku

Licha ya marufuku hiyo baadhi ya pikipiki hizo zinaendesha biashara ya usiku. Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia mauaji ya watu 12 kwa kipindi cha wiki moja mwezi wa Septemba 2016.

Kulingana na amri hiyo bodaoda hazipaswi kuhudumu baada ya saa tano usiku hadi saa kumi na moja asubuhi.

Mapema mwezi Januari mwaka huu zaidi ya pikipiki 40 zilinaswa usiku mjini Elodret kwa tuhuma za kutumika katika uhalifu usiku.

Afisa mkuu wa polisi Eldoret Magharibi, Bw Samuel Mutua, alisema msako dhidi ya pikipiki usiku ungalipo.

“Hatutaruhusu wahalifu waendelee kutumia pikipiki kuhaingaisha wananchi,” alisema Bw Mutunga.

Takwimu za polisi zaonyesha kuwa aslimia kubwa ya wahalifu ambao huangaisha wakazi wa mji wa Eldoret hutumia pikipiki kutoroka.