CBK yaonya Kenya itabanwa kuomba mikopo kimataifa
Na BERNARDINE MUTANU
Benki Kuu ya Kenya(CBK) sasa imeonya kuwa huenda serikali ikose kabisa uwezo wa kuchukua mikopo kutoka kwa mashirika ya kifedha ya kimataifa.
Benki hiyo ilitangaza hayo huku ikithibitisha kuwa Kenya ilipokea Sh202 bilioni kutokana na mauzo ya Eurobond II kutoka Benki ya Citi (New York) kupitia kwa Hazina Kuu ya Kitaifa Machi 12, 2017.
Kulingana na Gavana wa CBK Patrick Njoroge, labda ni wakati wa serikali kuzingatia kupata ufadhili wa miradi kwa njia zingine kuliko kutumia mikopo.
Dkt Njoroge alisema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Mipango na Biashara.
“Nafasi ni ndogo sana ya kukopa, ni wakati wa kuepuka kukopa kutekeleza miradi kama ule wa barabara ya Nairobi-Mombasa. Ni wakati wa kuacha wimbo wa kukopa ili kuwekeza,” Dkt Njoroge aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kipkelion Magharibi, Joseph Limo.
Gavana huyo alisema ufadhili usio wa mkopo haumaanishi tu ushirikiano kati ya serikali, mashirika na umma.
Alisema kukopa zaidi kutoka soko la kimataifa kutadhoofisha uwezo wa shilingi ya Kenya.