Habari Mseto

SENSA: Jamii za kuhamahama zaombwa kujitokeza kuhesabiwa

February 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na STEVE NJUGUNA

MBUNGE wa Laikipia Kaskazini, Sarah Lekorere ameziomba jamii za kuhamahama kuacha tamaduni ambazo zimekuwa zikizifanya kutopata habari kamilifu kuhusu idadi yao wakati wa sensa za kitaifa.

Mbunge huyo alisema kumekuwa na dhana kuwa jamii hizo huwa na watu wachache kutokana na habari finyu zinazotolewa wakati wa sensa.

Akiwahutubia wanahabari katika eneo la Doldol, Bi Lekorere alisema tamaduni za Wamaasai kuwazuia watoto kuhesabiwa zimekuwa zikiathiri idadi kamili ya watu katika maeneo hayo.

Aliapa kuwashinikiza viongozi kuwafunza wakazi kuhusu umuhimu wa shughuli hiyo na athari ya kutoa habari zisizofaa.

Alisema ugavi wa rasilimali za taifa huzingatia idadi ya watu walio katika eneo husika, akionya hatari ya jamii hizo kuendelea kutengwa kimaendeleo kwa kutotoa habari za kweli.

Mbali na hayo, alilalamika kwamba shughuli hiyo itafanywa wakati ambapo jamii nyingi zitakuwa zimeondoka katika maeneo yao ili kutafutia mifugo malisho.

Alieleza hilo kama hali ambayo huenda ikazuia wengi wao kuhesabiwa. Vile vile, aliomba watakaohesabu kuhakikisha mitambo itakayotumika haipati hitilafu zozote.