Cherargei aibua ubabe wa kisiasa kati ya Ruto na Moi
BARNABAS BII na WYCLIFFE KIPSANG
MATAMSHI ya Seneta wa Nandi Samson Cherargei ya kuwaonya wanaompiga vita Naibu Rais Dkt William Ruto yamezua upinzani mkali kati ya vyama vya Jubilee na KANU vinavyopigania umaarufu wa kisiasa katika eneo la eneo la Bonde la Ufa.
Akiwa katika hafla ya mazishi Kaunti ya Nandi, Bw Cherargei aliwaonya wanaompinga Dkt Ruto kuwa watachukuliwa hatua kali ambazo hakufichua na kuwataka wabadili nia na kumuunga mkono.
“Wale watu wanaendelea kumpiga vita Naibu Rais tunawaona. Ukimpinga Naibu Rais, unapigana nasi. Usifikiri kwamba hana wafuasi,” akasema Bw Cherargei.
Seneta huyo wiki jana alikamatwa na makachero kutoka Idara ya Upelelezi(DCI) lakini akawaachiliwa kwa dhamana ya polisi baada ya kuzuiliwa kwa saa kadhaa katika kituo cha polisi cha Central mjini Kisumu.
Viongozi wa Kanu sasa wanasema wapigakura hawafai kulazimishwa kumuunga Dkt Ruto wakidai ishara ziko wazi kuwa Jubilee haishabikiwi tena eneo hilo.
“Ishara ziko wazi kwamba umaarufu wa Jubilee unaendelea kudidimia huku wapigakura wengi wakikumbatia chama cha Kanu. Tumeanza kurindima ngoma yetu hadi mashinani ili chama kiwe dhabiti,” akasema Mshirikishi wa Kanu katika eneo la Bonde la Ufa, Bw Paul Kibet.
Naibu Rais na Mwenyekiti wa Kanu, Seneta Gideon Moi, wamekuwa na uhasama mkali wa kisiasa huku Bw Moi akiwapokea wanasiasa kutoka Jubilee ambao wamekuwa wakilalamikia udikteta wa viongozi wanaompigia upato ili aingie Ikulu mwaka wa 2022.
Viongozi wengine ambao pia hawamshabikii Dkt Ruto wamepata hifadhi katika Chama cha Mashinani(CCM) kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet, Bw Isaac Ruto.
Kama njia ya kutafuta uungwaji mkono, Bw Moi wiki jana aliwakaribisha viongozi wengi maadui wa Dkt Ruto nyumbani kwake Kabarak ambapo inakisiwa siasa za 2022 zilijadiliwa kwa mapana na marefu.
Waliohudhuria mkutano huo ni Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, Mbunge wa Moiben Sila Tiren, mbunge maalum wa ODM Wilson Sossion, Mbunge wa Tiaty William Kamket na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat. Mawaziri wa zamani Zakayo Cheruiyot, Musa Sirma, Frankline Bett, aliyekuwa Gavana wa Bomet Isack Ruto na mwanasiasa wa Uasin Gishu Zedikiah Bundotich(Buzeki) pia walikuwepo kwenye mkutano huo.
Bw Tolgos ambaye haelewani na Seneta wa kaunti hiyo Kipchumba Murkomen, mwandani wa Dkt Ruto, amewahi kunukuliwa akilalamikia namna wafuasi wa Naibu Rais wanavyowatisha viongozi wasiomuunga mkono.
Ingawa Bw Tolgos anashikilia kwamba bado yupo Jubilee na anawaheshimu Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta, amekuwa akimiminia sifa Bw Moi kama kiongozi shupavu ambaye anawaheshimu viongozi wengine.
“Nimependa sana jinsi Bw Moi amekuwa akiendesha siasa zake. Hamdunishi au kumchokoza kiongozi yeyote. Ana heshima kwa viongozi wengine kama tu mimi,” akasema Bw Tolgos akizungumza na Taifa Leo majuzi.
Bw Moi pia amekuwa akikutana na wazee wa jamii ya Kalenjin kama njia ya kuhakikisha anapata uungwaji mkono na kumpiga kumbo Dkt Ruto kwenye vita vya ubabe wa kisiasa katika Bonde la Ufa.