Habari Mseto

Chifu wa Kilimani ashtakiwa kughushi cheti

April 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

CHIFU wa Kilimani, kaunti ya Nairobi alishtakiwa  kwa kughushi cheti cha kumruhusu mwenye hoteli kuendeleza biashara katikati ya jiji.

Mwenye hoteli hiyo alidai leseni hiyo ilikuwa halisi. Leseni ambayo Bw Patrick Adagi Adira alidaiwa alighushi ilikuwa ya ada ya Sh61,000 inayotozwa wenye mikahawa.

Leseni hiyo Bw Adira alishtakiwa ilikuwa ya kumruhusu mwenye mkahawa wa Meriada Gardens Restaurant.

Cheti hicho anachodaiwa kughushi chifu huyo kilimruhusu mwenye hoteli hiyo kuendelea na kazi yake kwa kipindi cha mwaka wa 2017 pasi kusumbuliwa na askari wa kaunti ya Nairobi.

Bw Adira mwenye umri wa miaka 56 alikanusha mashtaka mawili aliyofunguliwa na afisi ya mkurugenzi wa  mashtaka ya umma (DPP) baada ya kuchunguzwa na tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC).

Cheti hicho nambari 1441411 kilichokabidhiwa Mkahawa huo Meriada Gardens kilidaiwa kilitolewa na afisi husika ya kutoa leseni kwa wafanya biashara ya kaunti ya Nairobi mnamo Agosti 2017.

Muda wa cheti hicho ungelitamatika Agosti 2018.

Hakimu alifahamishwa cheti hicho feki kilikabidhiwa afisa wa kaunti ya Nairobi Bw Johnson Akong’o mnamo Machi 16, 2018.

Bw Akong’o kutoka idara ya ukaguzi wa leseni za biashara ya kaunti alifika katika Mkahawa huo wa Meriada na kuomba akabidhiwe leseni ndipo akapewa leseni hiyo feki.

Mnamo Machi 18, 2018 hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi aliombwa na kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha atoe kibali kwa polisi cha kumtia nguvuni Bw Adira kujibu mashtaka ya ufisadi.

Bw Andayi alikubalia ombi la Bw Naulikha na kutoa kibali kwa maafisa wa polisi wamtie nguvuni mshtakiwa na kumfikisha kortini Machi 19, 2018.

Mshtakiwa hakufika kortini siku aliyotakiwa kufika kujibu mashtaka.