Chokoraa aliyepigwa risasi na polisi alilia haki
Bw Kaka Karanja anasema juhudi zake za kupata msaada kutoka kwa polisi zimegonga mwamba.Alisema alikuwa akitembea barabarani mwendo wa saa nne usiku Novemba 10 mwaka huu aliposikia milio ya risasi lakini kabla ya kujificha alikuwa amepigwa risasi pajani.
“Nililia lakini sikupata mtu wa kunisaidia, afisa mmoja wa polisi aliyeniona alikuja na kuagiza wenzake kunimaliza lakini kwa sababu kulikuwa na giza, nilijivuta na kujificha,” alisema.
Bw Karanja alisema vijana wenzake wa mtaani waliita ambulensi iliyokuwa ikipita na akapelekwa hospitali kuu ya Kenyatta.
“Hata hivyo, sikutibiwa kwa sababu sikuwa nimeandamana na maafisa wa polisi, hospitali ilinipatia dawa za kutuliza maumivu pekee,” alisema.
Alisema mama yake ambaye pia ni chokoraa alimtembelea lakini hakuweza kupata pesa za kulipa bili ya hospitali.Siku iliyofuata, aliondoka hospitali kwa miguu hadi barabara za Mlango Kubwa anakoishi.
Kulingana na Karanja, juhudi za kupata msaada kutoka kwa polisi zimegonga mwamba.
Alisema wiki jana, alienda katika kituo cha polisi cha Pangani akiandamana na vijana wenzake lakini hakuna aliyemsikiliza.
Alisema vijana wenzake mitaani wamekuwa wakitafuta pesa na kumnunulia tembe za kupunguza maumivu.Bw Karanja amekuwa na kidonda kwa wiki mbili bila matibabu.