COFEK yaikejeli CBK kushindwa kuzuia mikopo ya serikali
Na BERNARDINE MUTANU
Shirika la Kutetea Haki za Watumiaji Bidhaa (COFEK) limesifu wabunge kwa kukataa ombi la Benki Kuu ya Kenya kuondoa viwango vya mwisho vya riba kwa mikopo ya benki.
Shirika hilo limeshutumu CBK kwa kulenga kuondoa kiwango kilichowekwa kuwakinga wananchi dhidi ya viwango vya juu vya riba na benki.
Wakati huo, lilishutumu CBK kwa kushindwa kudhibiti serikali dhidi ya kukopa sana nchini, hali ambayo imeendelea kuwaumiza wananchi.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Cofek Bw Stephen Mutoro, Gavana wa CBK Dkt Patrick Njoroge amekataa kukutana na wawakilishi wa watumiaji bidhaa licha ya kushauriana mara kwa mara na wamiliki na wasimamizi wa benki.
Katibu huyo alisema COFEK haiungi mkono kudhibitiwa kwa viwango vya riba, lakini akaongeza kuwa Kenya ni maalum, hivyo, kudhibitiwa kwa riba kunahitajika.
Sheria ya kudhibitiwa kwa viwango vya riba ilitiwa sahihi na Rais Uhuru Kenyatta Agosti 24, 2016.
Alhamisi wiki jana, wabunge walikataa pendekezo la Dkt Njoroge la kuondoa viwango vya mwisho vya riba, ambavyo huwa ni asilimia nne, juu ya viwango vya ukopeshaji vya CBK, ambavyo ni asilimia 10.