Habari Mseto

Corona itakavyoitatiza Kenya kulipa madeni

April 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

VALENTINE OBARA na BENSON MATHEKA

MIKOPO tele iliyochukuliwa na serikali sasa imeitia nchi taabani kwani janga la corona linaendelea kuporomosha uchumi wa taifa.

Kufikia Desemba mwaka uliopita, Kenya ilikuwa inadaiwa zaidi ya Sh6 trilioni na wakopaji wa humu nchini na nchi za nje ikiwemo China, kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Benki ya Dunia imetoa wito kwa nchi na mashirika ambayo yalipatia Kenya mikopo yaahirishe ulipaji wa madeni hayo kwa vile hali ni mbaya kwa sasa.

Uchumi wa Kenya hutegemea sana sekta kama vile kilimo, utalii, kando na biashara nyinginezo ambazo sasa zote zimekwama kwa sababu ya masharti makali ya kupambana na janga la corona, ikiwemo kafyu na kufunga baadhi ya miji.

Shirika hilo la kimataifa lilisema hali sawa na hii inakumba mataifa mengi ya Afrika ambayo yalikuwa yakitegemea mikopo kimaendeleo.

“Nchini Kenya, inatarajiwa uchumi utaathirika kwa vile hakuna biashara zinazotoka kwa washirika wa taifa hilo, na pia ndani ya nchi,” ikasema ripoti.

Shirika hilo linasema kwamba, janga hilo la corona ndilo baya zaidi kuliko majanga matatu yaliyotangulia ndiposa uchumi wa ukanda huu wa kusini mwa jangwa la Sahara utadorora mno kwa mara ya kwanza katika miaka 25.

“Uchumi wa eneo la kusini mwa jangwa la Sahara utaporomoka na kukua kwa -2.1% hadi -5.1% mwaka huu kwa sababu ya janga la corona,” inasema ripoti ya Benki ya Dunia.

Kuhusu uwezo wa Kenya kupambana na corona, ripoti hiyo ilionyesha taifa hili lina nafasi bora barani Afrika.

Hii ni kutokana na kuwa, Kenya ni miongoni mwa nchi nne pekee kusini mwa jangwa la Sahara ambazo zimepitisha kiwango wastani cha ubora. Nchi nyingine ni Afrika Kusini, Uganda na Ethiopia.

Wakati huo huo, ilibainika janga la corona pia litapunguza idadi ya watu Afrika.

Ripoti hiyo inasema kuwa kasi ya ongezeko la watu katika eneo hili inatarajiwa kupungua hadi asilimia 2.7.

Kabla ya corona kuripotiwa katika eneo hili idadi ya watu ilitarajiwa kuongozeka kwa asilimia 3.6 mwaka huu.