Daystar kuchunguza kiini cha ghasia chuoni
Na LEONARD ONYANGO
CHUO Kikuu cha Daystar kimeunda jopokazi la kuchunguza vurugu za wanafunzi ambao zimekuwa zikishuhudiwa chuoni hapo mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Kampuni Simamizi ya Chuo cha Daystar Macmillan Kiiru alisema jopokazi hilo linaloongozwa na Profesa Henry Thairu litachunguza mvutano baina ya wanafunzi na usimamizi wa chuo hicho ambao umedumu kwa zaidi ya miezi minane.
Wiki mbili zilizopita, Seneti ya Daystar ilifunga kwa muda usiojulikana chuo hicho baada ya kuzuka kwa vurugu za wanafunzi.
Seneti ilifunga mabewa ya Nairobi na Athi River na ikaagiza wanafunzi kuondoka mara moja.
Chuo hicho kilifungwa baada ya bewa lake la Nairobi kugeuka kuwa ‘uwanja wa vita’ pale polisi walipoingia na kuwarushia wanafunzi vitoa machozi. Wanafunzi walikuwa wakiandamana kupinga hatua ya usimamizi wa chuo hicho kukosa kuhudhuria kikao baina ya viongozi wao na wajumbe wa Seneti.
Kikao hicho kilifaa kujadili ripoti ya uchunguzi kuhusiana na usimamizi wa fedha chuoni humo.
Wanafunzi wamekuwa wakilalamikia masuala mbalimbali kama vile kiwango duni cha kozi zinazofunzwa, ada ya juu inayotozwa ilhali wanafunzwa kozi duni, ukosefu wa vifaa vya kufundishia kati ya mambo mengineyo.
Wanafunzi wa uanahabari, kwa mfano, walilalamikia ukosefu wa studio ya redio au runinga pamoja na vifaa vinginevyo vya kufundishia.
“Jopokazi linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi na mapendekezo ndani ya siku 90. Tutatumia mapendekezo hayo kutatua mzozo ambao umekumba chuo hiki,” akasema Dkt Kiiru wakati wa uzinduzi wa jopokazi hilo katika Bewa la Valley Road la Chuo cha Daystar, Nairobi, Jumatano.
Aliagiza Baraza Simamizi la Chuo hicho kukabidhi jopokazi hilo ripoti kuhusiana na usimamizi wa fedha iliyozua vurugu baina ya wanafunzi na usimamizi wa chuo hicho, wiki mbili zilizopita.
Kaimu Naibu wa Chansela wa chuo hicho Profesa James Kombo aliahidi kushirikiana na jopokazi hilo linapoendesha uchunguzi wake.