EMMAH NJERI: Anawataka wasanii wakomeshe umbea na kupakana tope
Na JOHN KIMWERE
ALITAMANI kuhitimu kuwa askari polisi tangu akiwa mtoto lakini baada ya watumishi hao kuhusishwa na matukio mengi yasiofaa alijikuta akiyeyusha azimio hilo. Hata hivyo kwa sasa amezamia elimu ya kuhitimu kwa cheti cha diploma kama ripota na mtangazaji wa runinga.
Je nani huyu? Siyo mwingine ila Emmah Njeri anayeodhoroshwa kati ya waigizaji wa kike wanaovumisha tasnia ya filamu na muvi nchini.
Alianza kujihusisha na masuala uigizaji kanisani ambapo walikuwa wakishiriki muvi za injili ya Mungu.
Baadaye alijikuta akivunjika moyo akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili kwenye shule ya Hillcrest High Nakuru mwaka 2010.
”Mwaka 2016 nilipata tangazo moja kampuni ya Membly Film Production ilikuwa ikihitaji waigizaji ambapo niliposhiriki majaribio nilibahatika kufanya vizuri na kupewa nafasi kushiriki muvi moja nikiwa mhusika mkuu,” alisema na kuongeza kwamba hatua hiyo ilimtia motisha zaidi lakini hazikuwa shughuli rahisi.
Aliongeza ”Kiukweli hakuna jambo rahisi uigizaji pia hutesa wengi hasa kwa kulazimisha wengi wao kuweka kando shughuli zingine ili kutekeleza wajibu huo.” Dada huyu anawataka wengi ambao hupenda kuwaponda waigizaji kwa kuwafananisha na wahuni wafahamu uigizaji ni ajira kama nyingine.
Anakiri kwamba ni projekti iliyomfungulia mlango katika taaluma hiyo ambapo amefaulu kushiriki muvi nyingi tu ambazo zimepata mpenyo kurushwa kupitia runinga tofauti nchini ikiwamo Gikuyu TV, KTN, MNET na NTV.
Mwigizaji huyu anasema amepania kujituma kisabuni kuhakikisha amefikia levo ya kimataifa maana anataka kufanya kazi na waigizaji wa Hollywood.
Hapa Kenya anajipiga kifua kwamba anataka kumpiku Nice ‘Shiru’ Wanjeri aliyekuwa mwigizaji kwenye kipindi cha Auntie Boss cha ‘NTV’.
Kisura huyu anajivunia kufanya kazi ya uigizaji na brandi kadhaa hapa nchini ikiwamo Membly, Rollywood Production, Benover Entertainment kati ya zinginezo.
Barani Afrika anataka kufikia levo ya staa wa muvi za Kinigeria ‘Nollywood’ Ngozi Ezeonu aliyevumisha ulingo huo kupitia kazi zake kama: ‘Who owns the Child,’ ‘The Brave Wife’ na ‘Village Wahala’ kati ya zinginezo.
Emmah Njeri anayeamini anayo nafasi bora kutwaa tuzo katika masuala ya uigizaji siku sijazo anajivunia kushiriki muvi kama:’Women we Marry,’ ‘Cloud of Love,’ ‘Wicked Manager,’ ‘Prayerful Woman,’ ‘Debe igiri(debe mbili),’ ‘My Two Wives,’ na ‘Selina’.
Anashauri wanadada wenzake kwamba subira huvuta heri bila kuweka katika kaburi la sahau kuwa ‘vile huja haraka huisha haraka.’ Anawataka wakome kushushwa hadhi na wanaume pia wawe wanajiwekea kanuni ili kuwapa mwelekeo katika ulingo wa muvi.
Dada huyu anawataka wasanii wanaokuja wakomeshe umbea na maneno ya kuchafuana ili kufanikisha malengo yao katika uigizaji. Anasisitiza kwamba tasnia ya uigizaji nchini inapiga hatua kinyume na ilivyokuwa miaka iliyopita.