Familia za waliokufa Ethiopia zahangaishwa na mawakili
Na PHYLIS MUSASIA
MAWAKILI wakiwemo wa kutoka ng’ambo, wameanza kuziandamana familia za waliopoteza jamaa zao kwenye mkasa wa ndege ya Ethiopian Airlines mapema mwezi huu.
Familia za waathiriwa zinasema zimechoka kupokea simu kutoka kwa watu waonajitambulisha kama mawakili, huku wengine SMS zinazowaarifu waungane kwa pamoja na wenzao ili waweze kusaidiwa kupata fidia.
Hii ni licha ya Ethiopian Airlines kusema kuwa itawalipa fidia jamaa za watu 157 waliongamia Machi 10 kwenye ndege hiyo wakiwemo Wakenya 36.
Familia moja mjini Nakuru iliambia Taifa Leo kuwa, wiki jana ilitembelewa na kundi la watu waliojitambusha kama mawakili tajika Nairobi.
“Walitwambia wamekuja kuomboleza nasi na wamejitolea kutusaidia tupate fidia. Walipoondoka, nilipata ujumbe mwingine kwenye simu yangu uliotoka kwa mtu aliyejitambulisha kwa jina la Richmond. Alinieleza kuhusu kampuni yake ya uwakili, akidai imejitolea kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata fidia bila kulipia chochote,” akaeleza.
Aliongezea kuwa, ujumbe huo ulimtaka pia azifikishie ujumbe familia za waathiriwa wengine.
Familia nyingine iliyoomba kutotajwa, ilisema ilijiwa na kundi moja lililojitambulisha kufanya kazi na kampuni ya upelelezaji wa kibinafsi Nairobi, na kudai kuwa limepewa kibali cha kukusanya familia za waathiriwa wa mkasa huo wa ndege ili waweze kusaidiwa kwenye kesi ya fidia dhidi ya kampuni ya Boeing.
Mmoja wa familia hiyo alisema alipokea ujumbe kwenye WhatsApp uliosemekana ni kutoka kwa kampuni moja ya mawakili kutoka Marekani, ukidai kushirikiana na Ethiopia Airlines kuishtaki kampuni ya Boeing ili iwalipe waathiriwa fidia.
Waathiriwa wanaomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kuwalinda dhidi ya matapeli.
Wakili Steve Ogolla amekashifu vitendo hivyo vya mawakili, na kuomba familia za waathiriwa ziwe na uangalifu na kuwasilisha malalamishi yao haraka iwezekanavyo katika ofisi za sheria nchini kuhusu kuhangaishwa huko.
Familia hizo ziko kwenye majonzi zaidi baada ya kukosa kupata miili ya wapendwa wao, kwani iliharibiwa kiasi cha kutotambulika kwenye ajali hiyo.