Habari Mseto

FILAMU: Spellancer Nancy wa Inspekta Mwala alenga kuanzisha brandi yake

February 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

ANAJIVUNIA kufanya kazi nyingi chini ya kampuni tofauti tangu atambue kipaji chake katika uigizaji na kujitoma kwa tasnia ya filamu nchini miaka kumi iliyopita.

Kielimu, amehitimu shahada ya digrii kuhusu masuala ya biashara katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya  (MKU), na mwaka huu amejiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kusomea shahada ya uzamili. Aidha anamiliki brandi ya Spell Adecor Solutions ambayo husambaza bidhaa za wanawake na vijana.

Hata hivyo Spellancer Nancy Moraa mwenye umbo la kuvutia anapania kumiliki kampuni ya kuunda filamu za kuvutia humu nchini.

Anasema tasnia ya filamu inalipa ingawa haijapata mashiko ipasavyo hapa nchini. “Kenya imefurika waigizaji wengi tu wanaume na wanawake tatizo ni soko,” alisema alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali.

Anaongeza kuwa serikali inapaswa kujitokeza kuipiga jeki sekta ya filamu ili kutoa ajira kwa maelfu ya vijana waliojaliwa vipaji vya uigizaji.

Kama ujuavyo, katika taaluma yoyote kila mhusika huwa na malengo yake.Kisura huyu anapania kuibuka produsa wa kimataifa kufikia upeo wa msanii maarufu Likarion Wainaina.

”Kwenye kazi za msanii huyo, mimi huvutiwa na filamu maarufu iliyojulikana kama Supa Modo,” anasema.

Pia anataka kufanya kweli sawa na mwigizaji wa kimataifa katika Hollywood, Taraji Henson. Anasema kwa msanii huyo ambaye ni mwanamuziki, mchapishaji na mwigizaji hupendezwa na muvi ya kwake iitwayo ‘Cookie’.

Tangu mwaka 2012 Nancy huigiza katika kipindi maarufu nchini cha Inspekta Mwala ambacho hupeperushwa na runinga ya Citizen.

‘Poesha’ ndiyo filamu iliyomtambulisha katika sekta hiyo aliyoshiriki chini ya prodyuza John Karanja na kurushwa kupitia KBC TV. Kwenye ushiriki wake alikuwa mama mshamba kutoka Kaunti ya Kisii asiyefahamu lugha ya mijini.

Mwanzo alifanya na makundi mbalimbali kama Shangilia Africa na Planets Africa kabla ya kufifia. Mwaka 2015 alikuwa kati ya waigizaji walioshiriki filamu fupi chini ya Fourteen Ways iliyokwenda kwa jina ‘Subira’ na iliyoteuliwa kwenye mashindano tofauti.

Muvi hiyo iliteuliwa kwenye tuzo za Kalasha Awards kitengo cha Best Feature in Riverwood (Kenya), nchini Rwanda:Best feature in East Africa Films na Uganda: Best Feature film. 

Ameshiriki muvi tofauti ikiwamo: Bakile kupitia Yala Productions chini ya produsa Steve Ominde na Dennis Mitoko. Pia mwaka 2012 alishiriki kipindi kilichofahamika kama ‘Changing Times’ kupitia runinga ya KTN.

Pia ameshiriki ‘The chase,’ Social Teaching,’ ‘The rock,’ ‘Cobra Squad,‘ na ‘Naswa’ kati ya zingine.

Anasema kamwe hajutii kuigiza filamu nyingi akiwa mhusika mkuu ambaye nyakati zote hushiriki maovu kwani anafahamu usanii ni ajira kama nyingine.

”Nawashauri waigizaji wapya kwenye gemu kwamba hamna chochote hupatikana rahisi lazima wakaze kamba mithili ya mchwa,” anasema.