FLORENCE MUMBI: Runinga za Kenya zipunguze idadi ya filamu za kigeni
Na JOHN KIMWERE
ANAORODHESHWA kati ya waigizaji wa kike ibuka wanaolenga kuvumisha tasniaa ya filamu nchini. Aidha ni mwanamuziki wa kizazi kipya anayelenga kutesa siku za usoni kupitia tambo za kupangawisha wapenzi wa burudani.
Kando na uigizaji, analenga kuweka historia kwa kufanya kazi bomba za muziki. Kiukweli hajapata mashiko katika sekta ya burudani lakini anaamini muda utakapotimia hamna kitakachomzuia.
Hata hivyo, Florence Mumbi Karoki anasema itamlazimu ajitume zaidi maana hamna kizuri hupatikana kwa urahisi.
”Ingawa nilianza kushiriki uigizaji nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi kama taalamu nilianza mwaka uliyopita nilipojiunga na brandi ya Prima Pictures baada ya kutapatapa huku na kule bila mafanikio,” alisema na kuongeza kwamba analenga kukuza talanta yake zaidi maana anataka kuhakikisha ameibuka kati ya waigizaji watakaosaidia kupaisha tansia ya muvi nchini.
Anasema ilikuwa kama muujiza baada ya muvi aliyoshiriki kwa mara ya kwanza kupeperushwa kupitia runinga ya Inooro TV mwaka uliyopita.
”Nashukuru bosi wa Prima Pictures Roselyn Gacheru aliyeamini nina talanta tosha katika uigizaji maana nilikuwa nimehudhuria majaribio ndani ya miaka kadhaa bila kufaulu. Pia Prima Pictures huzalisha muvi ambazo hurushwa kupitia runinga ya Gikuyu TV na Kameme TV.
Mwigizaji huyu anawataka wamiliki wa runinga kupunguza vipindi vya filamu za kigeni na kuongezea vipindi vya kazi za wazalendo ili kufaidi waigizaji chipukizi.
Anasema kupitia brandi hiyo huzalisha muvi kwa kuzingatia maadili ya kijamii maana zinaweza kutazamwa kila mtu wakiwamo watoto. Binti huyu anajivunia kushiriki muvi kadhaa kama ‘Yari iria,’ na Marijuana’ kati ya zingine.
Katika muziki, mwimbaji huyu amefaulu kutunga na kurekodi fataki kadhaa ikiwamo ‘Niku Party,’ ‘With You,’ na ‘The Love’ ya injili. Amedokeza kuwa amezamia mpango wa kuachia nyimbo mpya hivi karibuni.
Kadhalika msanii hutumia uigizaji kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa akili (Bipolar illness) kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook. Akizungumza na ukumbi huu alisema kwamba alianzisha huduma hiyo alipogundua wapo watu ambao huteswa na ugonjwa huo kwa kutofahamu jinsi wanavyoweza kuhimili makali yake.
Kwa jumla kisura huyu anatoa mwito kwa wasanii chipukizi kutofunjika moyo baada ya kutokana na changamoto nyingi ambazo hupitia.
”Jambo lingine ni muhimu kwa wanaohisi wana talanta ya uigizaji, muziki au taalamu yoyote wanastahili kujizatiti pia kujiamini wanaweza bila kusikiza wanavyopondwa na wasiopenda maendeleo,” alisema.
Anawataka wasanii waliotangulia kuwashika mikono wenzao wanaokuja ili kuinua ulingo wa burudani ya muziki. Wakati hayupo mzigoni anasema hupenda kutazama muvi kuhusu mapenzi, drama na vituko.