Habari Mseto

Gavana Njuki ashtakiwa kwa kutimua wafanyakazi

April 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Wakili Davidson Warutere (kati) na wafanyakazi waliofutwa katika kaunti ya Tharaka Nithi wakiwa katika mahakama kuu ya Milimani Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Kuamua Mizozo ya Wafanyakazi (ELRC) Jumatano ilikubalia ombi la wafanyakazi waliofutwa kazi kumshtaki  Gavana wa Tharaka Nithi Bw Muthomi Njuki.

Jaji  Nzioki wa Makau alimruhusu wakili Davidson Warutere kuwashtaki Bw Njuki na wafanyakazi wengine wakuu katika kaunti hiyo.

Jaji huyo alifahamishwa na Bw Warutere kwamba wakuu hao wa kaunti hawakurudisha kazini wafanyakazi iliyowatimua kama ilivyoamriwa Nobemba 11 2017.

Wafanyakazi waliotimuliwa kazini na wengine kusimamishwa waliwasilisha kesi katika mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi tawi la Nyeri wakilalamika kwamba haki zao zimekandamizwa kwa kutolipwa licha ya kufanyia kaunti hiyo kazi.

Kesi hiyo iliposikizwa na Jaji Nzioki Makau  kaunti ya Tharaka Nithi iliamriwa iharamishe uamuzi wa kuwatimua kazini wafanyakazi  hao.

Lakini agizo hilo halikutekelezwa na Bw Warutere akawasilisha kesi nyingine akiomba Gavana Njuki pamoja na maafisa wengine wakuu katika kaunti hiyo wasukumwe jela kwa kipindi kisichopungua miezi sita kwa kudharau mahakama.

Na wakati huo huo wakili Jaji Makau alikataa kujiondoa katika kesi hiyo baada ya kuombwa ang’atuke kwenyes kesi hiyo kwa madai anapendelea upande mmoja.

Wakili Dkt Kamau Kuria anayetetea kaunti ya Tharaka Nithi alisema rufaa itawasilishwa kupinga uamuzi wa kuwarejesha kazini waliotumuliwa au kusimamisha.

Kesi hiyo itajwa Aprili 23, 2018 katika mahakama ya Nyeri baada ya Jaji Nzioki kukamilisha kuamua kesi jijini Nairobi.