Habari Mseto

Genge laiba bunduki za polisi wakati wa kafyu

March 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA WAANDISHI WETU

KITUO cha polisi eneo la Muhoroni, Kaunti ya Kisumu kilivamiwa Jumamosi usiku na wezi wakaiba bunduki tatu na risasi 155 wakati wa kafyu.

Wakuu wa usalama katika eneo la Nyanza walianzisha msako mara moja kutafuta silaha zilizoibiwa, wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Ujasusi (DCI) eneo la Nyanza, Bw James Kipsoi na Kamanda wa polisi katika eneo hilo, Dkt Vincent Makokha.Kisa hicho kilitokea huku wahalifu wakiendelea kuhangaisha wakazi mitaani na vijijini, polisi wakishika doria zaidi mijini.

Katika usiku wa Ijumaa na Jumamosi wakati wa kafyu, wezi walivamia nyumba za watu katika mitaa ya Lolwe, Migosi, Kenya Re na Carwash mjini humo.

Maduka pia hayakusazwa katika uhalifu uliotokea.Katika mtaa wa Lolwe, mtunzaji nyumba alivamiwa na genge lililomkatakata kwa panga kichwani na tumboni.

Bw Eric Kimwet Bii alikimbizwa hadi Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga ambapo alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Genge lingine lilivamia mitaa ya Migosi na Aliwa lakini likazidiwa nguvu na wakazi.

Katika Kaunti ya Kakamega, afisa wa jeshi la wanamaji nusura aporwe na jambazi aliyekuwa akiendesha boda boda katika eneobunge la Lurambi, usiku wa Ijumaa.Alisema alifanikiwa kumpiga jambazi huyo akamwacha akigaagaa kisha akaenda kupiga ripoti kwa polisi.

Ripoti za Victor Raballa, Rushdie Oudia, Benson Amadala na Shaban Makokha