Ghasia zatawala mchujo wa Jubilee Baringo
Na FLORAH KOECH
GHASIA zilikumba mchujo wa chama cha Jubilee eneobunge la Baringo Kusini kabla ya aliyekuwa katibu wa tawi la Baringo wa chama cha walimu nchini Charles Kamuren alipotangazwa mshindi Jumapili alasiri.
Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Bi Grace Kipchoim.
Miongoni mwa waliokuwa wakiwania kiti hicho ni mfanyabiashara anayeishi Amerika Mark Kiptoo, wakili Joseph Tarus na Eunice Lepario kutoka jamii ya Ilchamus.
Kwenye matokeo yaliyotangazwa na afisa aliyesimamia mchujo huo katika ofisi za naibu kamishna, Bw Kamuren alipata kura 13,882, Mark Kiptoo alikuwa wa pili kwa kura 8,919, Eunice Lepario alipata kura 999 naye Joseph Tarus alipata kura 431.
Uteuzi wa Jumamosi ulifanyika katika taharuki na madai kwamba kura hazikupigwa katika zaidi ya vituo 41 ambako masanduku ya kura hayakufika. Ilishukiwa kuwa afisa mmoja alitoweka na masanduku na karatasi za kura na kuyatumia katika vituo vingine.
Uchunguzi wa Taifa Leo katika kituo cha kujumlisha matokeo katika shule ya wavulana ya Marigat ulionyesha kuwa matokeo ya vituo ambavyo uteuzi haukufanyika yalitangazwa na afisa msimamizi Charles Bowen.
Ghasia zilitokea katika kituo hicho kila upande ukadai ulikuwa umeshinda na polisi wakalazimika kutumia nguvu kuwafukuza wafuasi waliokuwa na hasira kutoka ukumbini.
“Tunasimamisha shughuli hii na hatutaendelea. Tutapeleka masanduku ya kura katika ofisi ya naibu kamishna yakahifadhiwe hadi kesho ambapo tutashauriana na wawaniaji wote,” alitangaza Bw Bowen.
Jana wawaniaji walifanya mkutano kwa saa sita ambao wanahabari hawakuruhusiwa. Mambo yaliharibika Kiptoo na maajenti wake walipoondoka mkutano wakilalamika kuwa matokeo kutoka baadhi ya vituo yalibadilishwa.