• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Mchujo: Joho akosoa msimamo wa Shahbal

Mchujo: Joho akosoa msimamo wa Shahbal

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amewataka wanasiasa wanaowania tiketi ya ODM kukubali uamuzi wa chama kuteua atakayepeperusha bendera badala ya kushinda kuchafua jina lake majukwaani.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, wanawania tikiti ya chama cha ODM.

Hata hivyo, hivi majuzi, Bw Shahbal amejitokeza akikashifu chama cha ODM kwa ‘kuchagua viongozi watakaopeperusha bendera ya chama’ badala ya kupitia mchujo.

ODM haijaandaa mchujo wa wagombea wa ugavana Mombasa chanzo kilichosababisha mgawanyiko mkubwa katika chama hicho cha Bw Raila Odinga.

Akizungumza akiwa Mombasa, Bw Joho ambaye amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kutoonekana katika ulingo wa kisiasa kwa mwezi mmoja baada ya kuugua, aliwataka wanaotaka kumrithi kukoma kuchafua jina lake wakati wa mikutano yao na badala yake kuuza sera zao.

“Nataka kuwaambia wanaogombea Mombasa waniache. Hassan Joho hatawania kiti chochote hapa Mombasa. Popote unapoenda ni Joho… Joho… Joho. Una bahati sana siwezi tena kugombea ugavana sababu katiba hainiruhusu kwenda mihula zaidi ya miwili. Ningekuwa nagombea ugavana hapa Mombasa, ningekuonyesha kivumbi,” alisema huku akimtakia mrithi wake kila la heri.

Mwaka jana, Bw Joho alimtaja Bw Nassir kuwa mrithi wake.

Bw Nassir alipata uungwaji mkono kutoka kwa madiwani wote wa Mombasa isipokuwa mmoja na wabunge Mishi Mboko (Likoni), Badi Twalib (Jomvu) na seneta Mohammed Faki ambao wanaendelea kumpigia debe.

Bw Joho alisema amemaliza hatamu yake na anajipanga kwa mambo mengine ambayo hakuyataja.

Alisema amekuwa na nia nzuri ya kubadilisha maisha ya wakazi wa Mombasa na anafurahi kwamba ameifanikisha.

“Naona wengine wakijitangaza kuwa wakichaguliwa uongozini watabadilisha sekta ya afya. Mombasa tulianzisha upasuaji wa moyo, tunajivunia kuwa na hospitali spesheli ya kutibu saratani na wataalam waliohitimu na vifaa vya kisasa. Wewe utafanya nini ama wazungumza tu wala huelewi,” alisema.

Majuzi Bw Shahbal alitangaza kuwa amepata nafasi 10 za madaktari wa Mombasa kwenda Uturuki kusomea taaluma ya kutibu saratani.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa bwenyenye huyo kugombea ugavana. Mwaka wa 2013 aligombea kupitia tikiti ya Wiper na mwaka wa 2017 akajiunga na Jubilee.

akashindwa na Bw Joho wa ODM.

Bw Joho aliwarai wanasiasa wa Mombasa kuhubiri amani, umoja na upendo badala ya kuwagawanya wakazi kwa semi za uchochezi.

“Tuache hisia mbaya na kuchochea wananchi, ni vile tu nimefunga leo ningeongea sana..lakini ni Ramadhani,” alisema Bw Joho akiongeza kuwa anagonjea kwa hamu kuondoka mamlakani ili kiongozi mwingine achukue usukani.

Ata hivyo alimtaka mrithi wake kuhakikisha wanaendelea kazi nzuri atakayoiacha.

“Ninaweza kusimama kokote na kusema niliweza kufanya vyema hasa katika miradi ya maendeleo ambayo imeboresha maisha ya wakazi wa Mombasa hilo lilikuwa lengo langu kuu. Natumai mrithi wangu ataendeleza ruwaza yangu nzuri,” aliongeza gavana huyo.

Alichukua fursa hiyo kumpigia debe kinara wa ODM akiwasihi wapwani kumuunga mkono ili wnaufaike na serikali yake.

Aliwasihi wapwani kutokubali kudanganywa na Naibu wa Rais William Ruto akisema agenda yake si nzuri.

  • Tags

You can share this post!

Sekta ya kibinafsi kusaidia kuzima vikwazo katika biashara

Wiper yaahirisha mchujo kuruhusu maelewano

T L