Hamtakamatwa tena na polisi wa Uganda, serikali yahakikishia wavuvi Ziwa Victoria
Na BARACK ODUOR
SERIKALI imewahakikishia wavuvi katika Ziwa Victoria kwamba watapewa ulinzi dhidi ya kuhangaishwa na kukamatwa na maafisa wa usalama wa Uganda wanapoendeleza shughuli zao ziwani.
Kamanda wa Polisi katika Eneo la Nyanza, Bw Leonard Katana, alisema Idara ya Polisi wa Taifa (NPS) tayari imepeleka vifaa vya kutosha kutumiwa kukabiliana na ukosefu wa usalama ziwani na kulinda wavuvi.
“Tutapeana ulinzi katika maeneo yaliyo sugu kwa ukosefu wa usalama ili wavuvi wapate muda wa kutosha kuendeleza shughuli zao za uvuvi,” akasema Bw Katana.
Akizungumza wakati alipokutana na maafisa wa usalama na machifu wote wanaohudumu Kaunti ya Homa Bay, Bw Katana alisema wanalenga visiwa vya Remba, Takawiri, Kiwa, Ringiti na Migingo ziwani humo ambapo wavuvi wamekuwa wakilalamika kuhusu kuhangaishwa na kutishiwa na maafisa wa usalama wa Uganda.
Aliomba machifu na maafisa wengine wa usalama nchini wazidishe upigaji doria ili kuondoa wahalifu katika fuo za ziwa.
Aliahidi pia kuangamiza uuzaji wa pombe haramu katika visiwa vya Ziwa Victoria kwani zimesababisha maafa ya wavuvi wengi ziwani.
“Nimejitolea kuangamiza pombe haramu ambayo imeua wavuvi wetu wengi katika Ziwa Victoria,” akasema Bw Katana.
Mratibu wa serikali kuu katika eneo la Nyanza, Bw Morphat Kangi, aliomba wavuvi eneo hilo washirikiane kwa karibu na polisi ili kuwasaidia kuondoa wahalifu ambao wanatatiza usalama.
Haya yalitokea karibu mwezi mmoja baada ya wavuvi katibu 20 kutoka ufuo wa Kinda ulio kaunti ndogo ya Suba Kusini, kupigwa na kupokonywa taa zinazogharimu Sh70,000 na polisi wa Uganda.