Hamuoni aibu kudandia maandamano ya vijana wa Gen Z? UDA yauliza Azimio
CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimeshutumu muungano wa Azimio la Umoja kwa kudandia maandamano ya Gen-Z kuendeleza masilahi yao yasiyoakisi matakwa ya vijana hao na Wakenya kwa ujumla.
Kwenye taarifa Jumatano, Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala alisema ni aibu kwamba wanasiasa fulani, waliokataliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu uliopita, wanapania kujipatia umaarufu wa kisiasa kutokana na hali inayoshuhudiwa nchini wakati huu.
“Huku tukiwapongeza Gen-Z kwa kudumisha amani wakati wa maandamano, inahuzunisha kuwa watu fulani, wenye ubinafsi, ndani ya tabaka la wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambao wameteka maandamano haya kuendeleza malengo yao ya kibinafsi,” akasema.
Bw Malala alisema hayo saa chache baada ya mmoja wa vinara wa Azimio, Kalonzo Musyoka kumtaka Rais William Ruto kutia saini Mswada wa IEBC utakaofanikisha uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili iandae uchaguzi wa mapema.
“Tayari Wakenya wameonyesha kwamba hawana imani na serikali hii. Ndiposa tunamhimiza Rais kutia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ili Wakenya wapate nafasi ya kurudi debeni kuwachagua viongozi wapya kuendesha serikali.
“Wabunge sasa wanaogopa kuenda bungeni au katika maeneo yao ya uwakilishi, kwa hivyo raia wapewe nafasi ya kuwachagua wabunge wengine,” Bw Musyoka akasema kwenye kikao na wanahabari, Nairobi.
Mnamo Jumanne, chama cha ODM kiliitaka serikali ya Rais William Ruto kuwajibikia vifo na majeruhi kutoka na maandamano hayo ambayo yamedumu kwa majuma matatu.
Kulingana na Tume Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinafamu Nchini (KNCHR) watu 39 walikufana wengi 361 wakajeruhiwa kutokana na ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji.
Hata hivyo, katika taarifa yake, Bw Malala aliwamiminia sifa maafisa wa polisi kuwa kutotumia nguvu kupitia kiasi walipokabilia na “wahalifu waliozua fujo na kupora mali wakati wa maandamano ya amani yaliyoitishwa na vijana wa Gen-Z.”