Habari Mseto

Hisia kali kuhusu pendekezo watoto wa miaka 16 kuruhusiwa kufanya ngono

March 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

PENDEKEZO la Majaji wa Mahakama ya Rufaa kuwa umri wa watoto kuruhusiwa kujihusisha na ngono unafaa kupunguzwa kutoka miaka 18 hadi 16 limeanza kuvutia hisia kali, baadhi ya washikadau wakilipinga.

Majaji Roselyn Nambuye, Daniel Musinga na Patrick Kiage wakitoa uamuzi walisema kuwa umri wa watoto kuwa na haki ya kujiamulia kufanya mapenzi kwa hiari unafaa kupunguzwa, kutokana na visa vingi ambapo wanaume wamefungwa jela kwa makosa ambayo walioshtakwa kuwanajisi walikuwa wameelewana.

Majaji hao walisema hayo walipokuwa wakitupilia mbali kifungo dhidi ya mwanamume aliyefungwa miaka 15 jela, kwa kumtia mimba msichana wa miaka 17.

Walisema taifa linafaa kujadili kuhusu kupunguzwa kwa umri huo kwani wanaume wengi wanaozea jela, wakati walihukumiwa kwa kuwanajisi wasichana ambao walikuwa na hiari na walikaa kama watu wazima.

Lakini mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kuhusu Elimu Julius Melly jana alipinga pendekezo la Majaji hao, akisema miaka 16 ni umri mdogo kwa mtoto kuruhusiwa kujiamulia, kwani hilo litaathiri elimu.

“Watoto wengi wa miaka 16 wako aidha kidato cha pili ama cha tatu na hata kwa wanochelewa masomoni shule za msingi. Hivyo kuruhusu watoto wa kiwango hicho kujiamulia tutaanza kushuhudia visa vya wanafunzi kupata mimba na kuacha masomo ovyoovyo,” akasema Bw Melly, ambaye pia ni mbunge wa Tinderet.

Mbunge huyo alisema umri huo unafaa kusalia miaka 18 kama ilivyo sasa, kwani watoto wengi huwa wamekamilisha masomo ya shule za upili, wamekomaa kutosha na wameanza kuelewa maisha vyema.

Lakini majaji hao, katika uamuzi wao, walikuwa wamesema “Inawezekana wakawa hawajafikisha umri wa ukomavu lakini wanaweza kuwa wamefikisha umri wa kujiamulia kizuri na kibaya kwa maisha na mili yao.”

Majaji hao walisema sheria kuhusu makosa ya kingono dhidi ya watoto sasa inafaa kukaguliwa vyema na kurekebishwa ili kutatua baadhi ya changamoto, ambazo zimewapeleka watu wengi gerezani.

Mjadala huo umeibuka wakati kumekuwa na visa vya mara kwa mara vya wanaume, ikiwemo walimu, kushtakiwa kwa kushiriki ngono na wanafunzi ama watoto wengine wa umri huo, ama wa chini.

Baadhi ya wazazi aidha wanahoji kuwa umri wa miaka 16 ni wa chini kwa mtoto kuwa na uhuru wa kujiamulia, wakihofia watoto wengi watafanya maamuzi ya kupotosha katika maisha yao.