Hisia mseto Twitter kuhusu filamu ya 'Sincerely Daisy'
NA WANGU KANURI
Filamu ya Sincerely Daisy iliyoongozwa na mwigizaji maarufu Nick Mutuma ilionyeshwa kwa mtandao wa filamu wa Netflix huku ikiwa filamu ya pili nchini Kenya iliyopata kuonyeshwa kwenye Netflix baada ya Poacher.
Hata hivyo, Wakenya walifurika katika mtandao wa Twitter na kutoa maoni yao kuhusu kazi hiyo, wengi wakiisifia na wengine kuikejeli. Taifa Leo Dijitali ilikusanya baadhi ya hisia za wapenzi wa burudani:
“#SincerelyDaisy kama Mkenya, nimejionea fahari. Kama mwigizaji, nimejionea fahari mara dufu. Yaani ninakosa hadi maneno ya kueleza ninavyohisi. #SincerelyDaisy ni filamu iliyo nzuri na iliyoigizwa vyema,” akasema @shiviske
@NamasakaT alisema ni filamu nzuri. “Nenda ukaitazame sio tu kwa kuwa utakuwa ukiunga mkono talanta zilizopo Kenya bali kwa kuwa itaufaa muda wako.”
“Nimeitazama filamu ya #SincerelyDaisy ili kuunga mkono makala ya Kenya lakini jinsi filamu hiyo ilivyoandikwa haikufikia viwango vya kimataifa,” akaandika @peshnny
“Niliitazama filamu ya #SincerelyDaisy wikendi na iliniburudisha lakini jinsi filamu ilivyoandikwa haikuwa na uhalisi wowote jambo ambalo nilitarajia kutoka kwa waandishi chipukizi wa filamu. Hali kadhalika, kuna jambo moja ambalo lilinisumbua nilipokuwa nikitizama filamu hiyo- ukosefu wa kelele za mbali,” akadai @Miz_Soraya
“Iwapo unatafuta filamu ya kutazama Ijumaa hii, filamu yenye asili ya Kenya #SincerelyDaisy itakuwa ikionyeshwa kwenye mtandao wa filamu wa Netflix. Filamu hii imeongozwa na @nickmutuma, SincerelyDaisy ni filamu ya kwanza ya Kenya kuonyeshwa kupitia mtandao huuwa Netflix,” akasifia @sinemafocuske
“Hata ingawa tumefurahia kuitazama filamu hii, kwa kiwango fulani filamu hiyo haikuridhisha kwa kuwa uandishi wa makala yake haujanoga. Uandishi wa filamu uliokita kambi katika mapenzi, umasikini na uongo ni uandishi unaofanana na kila filamu iliyotengenezewa nchini. Hali kadhalika, SincerelyDaisy inaonyesha mwelekeo na kuwatia moyo waandishi wa filamu katika nchi ya Kenya,” akataja @Don Kogai
SincerelyDaisy ilionyeshwa kwenye Netflix mnamo Oktoba 9 na ni filamu yenye muda wa saa moja na dakika 27 na imetafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza huku asilimia 70 ya uigizaji wake ukiwa katika lugha ya Kiswahili.
Daisy ambaye jina lake halisi ni Ellah Maina, ni msichana aliyemaliza masomo yake ya Kidato cha Nne na ambaye anaangazia kuendeleza masomo yake ng’ambo.
Hata hivyo, mambo yanamwendea kombo Daisy pindi tu anapogundua kuwa familia yake haina uwezo wa kifedha ya kugharamia masomo yake kule ng’ambo.
Isitoshe, anakumbana na changamoto za maisha zinazofanya uhusiano wake na familia yake, mpenzi wake na marafiki zake kuwa kwenye njia panda.
Filamu hii inagusia vigezo muhimu katika maisha ya kila mwanadamu; familia, marafiki, maono ya mtu husika na kuzoroteka kwa uchumi.