Hoja ya Jicho Pevu kupinga ada za mochari yapitishwa bungeni
Na CHARLES WASONGA
HOSPITALI za umma sasa hazitakuwa zikiitisha malimbikizi ya ada za matibabu kwa wagonjwa watakaofariki wakitibiwa katika hospitali za umma za rufaa, ikiwa serikali itatekeleza hoja iliyopitishwa na wabunge Jumatano.
Kulingana na hoja hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Nyali, Mohammed Ali almaarufu Jicho Pevu, haifai kwa hospitali hizo kukatalia miili ya wagonjwa waliofariki baada ya jamaa zao kushindwa kulipa malimbikizi ya gharama za matibabu.
“Baada ya kupitishwa kwa hoja hii, sasa serikali inapasa kuhakikisha kuwa Wakenya wenye mapato ya chini kama mama mboga, makondakta wa matatu na wengineo, wanaruhusiwa kuchukua miili ya wapendwa wao wanaofariki wakipokea matibabu bila kutozwa ada za matibabu na utunzaji wa miili,” akasema Bw Ali.
Kumekuwa na visa vingi vya Wakenya, haswa wa mapato ya chini, kuzuiwa kuchukua miili ya wapendwa wao wanaofariki wakitibiwa katika hospitali za rufaa za umma kama vile Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) na ile ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) Eldoret zinazosimamiwa na serikali ya kitaifa.
Sasa ni wajibu wa Kamati ya Bunge kuhusu Utekeleza inayoongozwa na Mbunge wa Narok Kaskazini, Moitalel Ole Kenta kuhakikisha kuwa serikali inatelekeza pendekezo hilo la wabunge ndani ya muda wa siku 60.
Akichangia hoja hiyo wiki jana, Mbunge Mwakilishi Wanawake wa Nairobi, Esther Passaris, alisema ni kinyume cha Katiba kwa hospitali za rufaa kukataa kuachilia maiti, ilhali Wakenya wengi ni maskini na hawawezi kumudu gharama ya ada za hospitali.
“Kulingana na kipengee cha 43 ya Katiba, ni haki ya kila Mkenya kupata huduma za matibabu, inayojumuisha haki ya kupata utunzi wa kimatibabu kwa wagonjwa waliolazwa haswa katika hospitali zinazosimamiwa na serikali kuu. Kwa hivyo ni kinyume cha Katiba kwa hospitali hizi kuendelea na mtindo huu wa kuzuia miili ya waliokufa wakidai bili zilipwe,” akaaleza.
Bw Ali, kupitia hoja hiyo, pia aliitaka serikali kudhibiti ada ya mochari katika hospitali za umma, akisema ada zinazotozwa wananchi wakati huu ni za juu mno.