Hoteli Kisumu zavuna matunda ya muafaka kwenye ziara ya Rais
Na ELIZABETH OJINA-250
MIKAHAWA ya kifahari jijini Kisumu imevuna pakubwa kutokana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mpango wa Afya kwa Wote hapo Alhamisi.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta kuzuru kaunti hiyo baada ya kuingia kwa muafaka baina yake na kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga, ambao wamiliki wa hoteli walikiri umewaletea mapeni.
Kulingana na mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Hoteli wa Magharibi mwa Kenya Bw Robinson Anyal, hoteli kama Acacia, Imperial na Sovereign zilijaa wateja.
“Hoteli kuu tatu zimejaa. Acacia ina vitanda 91, Imperial 80 na Sovereign 40. Paliposalia na nafasi labda ni Grand Royal Swiss Hotel,” akaambia Taifa Leo.
Aliongeza, “Kando na malazi katika Hoteli ya Acacia, biashara ya vyakula imenoga. Tunatarajia mikahawa mingine hapa jijini kushuhudia kuongezeka kwa mapato.”
Alisema ziara ya Rais itafungua nafasi za biashara kwa mikahawa kama Kakwacha, Tilapia Resort na mikahawa mingine inayouza samaki eneo la ufuo wa Lwang’.
“Biashara ya teksi pia itaendelea kuvutia wateja katika siku mbili zijazo kufuatia ziara ya Rais,” akasema.
Alikariri kuwa ziara hiyo inapiga jeki biashara ya hoteli, huku nyingi zikitamatisha biashara ya kukodisha maeneo ya hotuba.
“Ziara ya Rais ni hakikisho kuu kwamba jiji la Kisumu li salama. Biashara ya kumbi za hotuba inaendelea kutamatika. Hoteli nyingi zinategemea watalii wa humu nchini,” akasema.
Meneja wa Hoteli ya Acacia Duncan Mwangi alisema hoteli hiyo ilipata wateja wengi zaidi wiki hii kutokana na ziara hiyo.
“Ziara ya Rais imeleta imani kuu na kuyeyusha hisia na fikra potovu ambazo watu wamekuwa nazo kuhusu Kisumu. Tunatarajia kuwa itaimarisha utalii wetu. Kwa hakika, muafaka wa Bw Kenyatta na Bw Raila umezaa matunda,” akasema.