Habari Mseto

Huenda bei ya bidhaa ikashuka baada ya hatua hii

April 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Shirika la Umeme nchini, Kenya Power, limeingia katika mkataba na Chama cha Watengenezaji wa Bidhaa (KAM) kuhakikisha uzalishaji na utumiaji mzuri wa umeme.

Hatua hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa kampuni za utengenezaji wa bidhaa ili kupunguza bei ya bidhaa zilizotengenezewa humu nchini na kukuza uwekezaji katika sekta ya utengenezaji wa bidhaa.

Kenya Power pia imejitolea kutoa kawi ya gharama ya chini kwa viwanda kwa kuwekeza zaidi katika utengenezaji wa mfumo wa usambazaji umeme ili kupunguza visa vya kupotea kwa umeme nchini.

“Kampuni hii inatambua juhudi za KAM katika kupigia debe miradi inayotumia vyema umeme miongoni mwa wanachama wake. Tumejitolea kushirikiana ili kuweka gharama chini,” alisema Meneja Mkurugenzi wa Kenya Power Dkt Ken Tarus jana.

Alisema kampuni hiyo itaendelea kuimarisha na kugeuza katika mfumo wa kidigitali opereshenu zake ili kuongeza uwezo wa kupata umeme ili kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.