Habari Mseto

Idara ya polisi wa trafiki yavunjwa kuzima hongo barabarani

March 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

INSPEKTA Jenerali wa polisi, Bw Joseph Boinnet, amevunjilia mbali idara ya polisi wa trafiki na kutangaza kuwa, afisa yeyote wa polisi atakuwa akipewa jukumu la kuelekeza magari barabarani.

Mwongozo mpya uliotolewa na Bw Boinnet wasema wakuu wa vituo vya polisi (OCS) ndio watakuwa na mamlaka ya kuongoza usimamizi wa masuala ya trafiki. Jukumu hilo limekuwa likisimamiwa na makamanda wa trafiki ambao sasa watapewa majukumu mengine.

Hatua hii imechukuliwa miezi michache baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuahidi kukabiliana vikali na tabia ya polisi wa trafiki kuitisha hongo kutoka kwa waendeshaji magari.

Idara ya polisi wa trafiki imekuwa ikiongoza kwenye ripoti za tafiti mbalimbali kuhusu ufisadi nchini.

Katika siku za hivi majuzi, maafisa hao wamebuni mbinu mpya za kukusanya hongo ikiwemo kutumia vijana kuwachukulia pesa hizo kutoka kwa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma.

Ripoti zinaonyesha kuwa, ukusanyaji wa hongo umekuwa ukifanywa kwa mpangilio hivi kwamba, maafisa wa vyeo vya chini walio barabarani hugawa kile wanachokusanya na wakubwa wao ambao huwatuma kazini.

 

Hongo ya Sh3 bilioni

Lalama kutoka kwa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) ni kuwa, wao hupoteza karibu Sh3 bilioni kila mwaka ambazo hupeanwa kama hongo kwa polisi wa trafiki.

Tabia hii huwa imelaumiwa kuchangia ajali za barabarani ambapo raia wengi wamepoteza maisha yao.

Agizo la Bw Boinnet pia limetokea miezi michache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA) waondoke barabarani mapema mwaka huu ili kuachia polisi jukumu la kusimamia trafiki.

Rais Kenyatta alitoa amri hiyo kufuatia ajali nyingi za barabarani zilizoshuhudiwa mwishoni mwa mwaka uliopita.

Kuna uwezekano maafisa wa polisi wa trafiki watapinga hatua iliyochukuliwa na Bw Boinnet hasa kwa msingi kwamba, si polisi wote wanafahamu vyema kuhusu mbinu za kusimamia trafiki na sheria zinazohitaji kufuatwa.