Habari MsetoSiasa

IEBC yakagua nusu ya saini za 'Punguza Mzigo'

June 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imekagua nusu ya saini ambazo ziliwasilishwa na chama cha Thirdway Alliance, chini ya mpango wa ‘Punguza Mzigo’ unaoshinikiza mageuzi ya katiba.

Chama hicho, ambacho kinaongozwa na Dkt Ekuru Aukot kinataka katiba ya sasa kufanyiwa mageuzi kwa njia ya kura ya maoni, kikishikilia kuwa utekelezaji wake ni ghali sana kwa mlipa ushuru.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, mwenyekiti wa tume hiyo Bw Wafula Chebukati alisema kuwa kufikia sasa, wamekagua saini 500,000 kati ya 1. 4 milioni ambazo ziliwasilishwa na chama hicho.

Ukaguzi huo unaendeshwa na makarani 125 chini ya wasimamizi wa maafisa 24 wa tume hiyo, wenye utaalamu kuhusu masuala ya uchaguzi.

“Mchakato huu unaendelea bila tatizo lolote. Kufikia sasa, tumekagua nusu ya saini zote zilizowasilishwa. Tunatarajia kumaliza mchakato huo katika

majuma kadhaa yajayo,” akasema Bw Chebukati bila ufafanuzi Zaidi.

Chama hicho kiliwasilisha saini hizo mnamo Februari 21 baada ya kuzikusanya katika kaunti zote 47.

Utaratibu huo ulitarajiwa kumalizika mnamo Mei 9, lakini ukachelewa katika kile tume ilisema ni ucheleweshaji wa fedha za kuendesha ukaguzi huo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa baada ya mchakato huo kukamilika, tume itawasilisha rasimu ya Mswada wa Kura ya Maoni kwa bunge za kaunti 47 zote ili kujadiliwa.

Bunge hizo zitakuwa na hadi miezi mitatu kuujadili. Baada ya hapo, tume itahitaji mswada huo kupitishwa na kaunti angaa 24.

Baadaye, utawasilishwa kwa Bunge la Kitaifa na Seneti ili kujadiliwa rasmi. Kulingana na Bw Chebukati, uamuzi wa mabunge hayo mawili ndiyo utakuwa sauti ya mwisho ya ikiwa mswada huo utapita au la.

Baadhi ya mapendekezo ya mswada huo ni kupunguzwa kwa idadi ya wabunge kutoka 416 hadi 147, kufutiliwa mbali kwa maeneobunge 290 ambapo badala yake, kaunti zote 47 zitatumika kama maeneobunge.

Wananchi watawachagua wawakilishi wao katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Mswada huo pia unalenga kupunguza kiwango cha fedha kinachotumika katika kuwalipa mishahara wafanyakazi wa serikali na gharama ya maandalizi ya chaguzi kuu.

Na licha ya mchakato huo kuendelea bila Afisa Mkuu Mtendaji na baadhi ya makamishna, Bw Chebukati alisema kuwa hilo haliathiri shughuli zake hata kidogo.

Tume hiyo haijakuwa na afisa mkuu mtendaji maalum tangu kufutwa kazi Bw Ezra Chiloba mwaka uliopita, ambaye alishikilia nafasi hiyo. Kando na Bw Chebukati, tume hiyo pia imekuwa na makamishna wawili pekee, wakiwemo Prof Abdi Guliye na Bw Boya Molu.

“Hakuna pengo lolote katika tume, kwani tuna kaimu afisa mkuu mtendaji ambaye anasimamia baadhi ya majukumu yake muhimu,” akasema.

Mchakato wa kumtafuta afisa mkuu mpya mtendaji umeanza, ambapo watu kadhaa wameorodheshwa kuhojiwa.