Habari Mseto

Ikulu yakemewa kuzidi kutetea mradi wa nyumba

May 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

WAKENYA wameikaanga Ikulu kwa kuendelea kutetea mpango wa kuwakata watu pesa ili kufadhili ujenzi wa nyumba za bei nafuu, wakiitaka serikali kutupilia mabli mpango huo ambao unaonyesha dalili zote kuwa hautafanikiwa.

Ikulu Jumatatu iliamkia kutetea mpango huo, ikisema kuwa hata ikiwa mtu hatafanikiwa kupata nyumba, atarudishiwa pesa zake baada ya miaka 15.

“Mpango wa kukata pesa za kufadhili ujenzi wa nyumba ni uwekezaji. Ukichanga pesa hizo kisha baada ya miaka 15 ukose kupata nyumba kupitia mpango huu utarudishiwa pesa zako,” Ikulu ikasema.

Wakenya, hata hivyo, waliupokea vibaya ujumbe wa Ikulu, wakiendelea kukemea mpango huo kuwa usio na nia njema kwa watu na ambao hauna uwazi.

“Kwanini serikali lazima ishurutishe watu kushiriki katika mpango huu ilhali tayari wana nyumba?” akauliza Nickleonard Juma.

Wakili Kegode naye alisema ikiwa huo ndio mpango wa serikali “basi muufanye mpango huo kuwa hiari ili wasiotaka kushiriki watumie mbinu nyingine za uwekezaji ambazo watajiamulia.”

Wengine waliendelea kutoa hisia ambazo zimekuwapo tangu mwanzoni, wakishangaa ina faida gani kwa serikali kumtoza mtu pesa kwa lazima kufadhili ujenzi wa nyumba wakati tayari amechukua mkopo kujijengea mwenyewe na bado anakatwa.

“Si haki kulazimishia Wakenya mradi huu, tayari ninajijengea nyumba yangu, mnataka niitupe ama nipeane kama zawadi nisubiri nyumba nitakayojengewa na serikali?” akashangaa njue alex.

“Sasa iweje mtu achange pea kwa miaka 15 kisha akose nyumba? Achaneni na huu mpango, watu waachwe wawekeze na mashirika yao ambapo watajenga kwa miaka mitatu,” akasema Joshua.