IRENE KIENDI: Mwigizaji wa Viusasa nguli wa filamu za Kikamba
Na JOHN KIMWERE
NI kati ya wasanii wanaokuja katika tasnia ya uigizaji hapa Kenya. Anaamini ana talanta tosha kufanya kweli katika burudani ya maigizo.
Hata hivyo alitamani kuhitimu kuwa mwanahabari tangia akiwa mtoto. Bila kuweka katika kaburi la sahau anakumbuka mara kwa mara alikuwa akifanya mazoezi ya utangazaji akisoma Shule ya Msingi ya Kwa Kiketi katika Kaunti ya Makueni.
Ingawa ndiyo mwanzo wa ngoma, anasema hana la ziada bali kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha nyota yake imeng’aa katika tasnia ya filamu nchini.
Alianza kujituma kwenye masuala ya maigizo mwaka 2010 baada ya kutamatisha elimu ya sekondari lakini anapania makuu.
Je ni nani huyu? Siyo mwingine bali ni binti mcheshi si haba, Irene Mutete Kiendi. Unajua nini? Hayo tisa, umi kitaaluma binti huyu ni mwigizaji, pia amehitimu kama mwalimu na mwanahabari.
Kadhalika, anajivunia kipaji cha ucheshi maana kando na uigizaji pia hualikwa kuchapa kazi kama mratibu wa sherehe (MC) kwenye hafla mbali mbali ikiwamo harusi kati ya zingine.
“Siwezi kusahau nilishawishiwa na Steve Maunda mwanaye aliyekuwa mtangazaji mahiri Jacob William Maunda,” anasema na kuongeza kwamba alichukua hatua hiyo baada ya kutambua ucheshi wake.
Binti huyu ambaye katika maigizo anafahamika kama ‘Ngene’ na ‘Msweetest’ ndani ya miaka miwili amefaulu kushiriki filamu tofauti ambazo hurushwa kupitia stesheni ya Citizen.
Mwaka uliopita na mwaka huu ameshiriki mara mbili filamu za kipindi maarufu cha ‘Inspekta Mwala’ ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.
Amekuwa muhusika mkuu kwenye filamu za ‘Viusasa’ ambazo hurushwa na kituo hicho. Baadhi yazo zikiwa ‘Katuililangi (kurukaruka),’ ‘Katenzoni (Hauna aibu)’ kati ya zingine.
”Kwa sasa nimezamia kukuza talanta yangu katika uigizaji ingawa kwa miaka kumi nilifanya kazi kama mwalimu nikifunza shule za msingi eneo la South B Nairobi,” anasema.
Analenga kumakinika katika tasnia ya filamu na muvi kufikia hadhi ya mwigizaji hodari, Sarah Atieno ambaye kisanaa anafahamika kama Lavender. Aidha anataka kujikaza kufuata nyayo za veretani na staa wa filamu za Kinigeria, Mercy Johnson.
Anapania kuibuka kati ya mastaa bora katika uigizaji nchini na Afrika mashariki kwa jumla. ”Napenda kujifunza zaidi kwa wengine pia kushirikiana na wenzangu kujadili masuala tofauti katika harakati za kujiendeleza,” alidokeza.
Kwa ushirikiano wake na wenzake wawili wanatengeneza filamu ‘Wimbimbi’ huku wakiendelea kusaka soko. Pia akishirikiana na waigizaji wengine wawili wamejitwika jukumu la kutengeneza muvi fupi na kuzitupia kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube kwenye jiitihada za kutangaza talanta yao.
Mcheshi huyu anapenda kuketi kutazama filamu za Nigeria na Tanzania pia kusoma vitabu vya riwaya. Vile vile yeye hubadilishana mawaidha na marafiki mbalimbali.