Habari Mseto

Jaji Kihara na Haji waidhinishwa na kamati ya bunge

March 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA
KAMATI ya Bunge kuhusu Uteuzi (JLAC) imemwidhinisha Rais wa Mahakama ya Rufaa, Jaji (mstaafu) Paul Kihara Kariuki kuwa Mwanasheria Mkuu mpya.
Na kwenye ripoti iliyowasilisha bungeni Jumanne alasiri kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini Bw William Cheptumo pia ilipendekeza kwamba Bw Noordin Mohammed Haji ateuliwa kuwa Mkurugenzi Mpya wa Mashtaka ya Umma (DPP).
Kamati hiyo  inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ilisema kuwa Jaji Kariuki alitimiza mahitaji yote yaliyoko kwenye Katiba kwa mtu kuteuliwa kwa wadhifa huo.
Kamati hiyo ilisema: “Tumedhihirisha kuwa anafahamu sheria kwa undani kando na kuelewa mazingira ambamo atahitajika kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu .”
Wabunge waliridhika kuwa Jaji Kariuki sio raia wa mataifa mwili tu, pia ana tajriba pana katika taaluma ya uanasheria na hajashikilia wadhifa wote katika chama cha kisiasa.
Ingawa bunge la kitaifa lina muda wa siku 14 kujadili ripoti ya kamati hizo, wabunge wanatarajiwa kukamilisha mjadala kuhusu ripoti hiyo kufikia Alhamisi wiki ijayo kabla ya wabunge kwenda likizo ya fupi ya siku 10.
Endapo Jaji Kariuki na Bw Haji watapitishwa na wabunge, Rais Uhuru Kenyatta atawateua rasmi kabla ya kuapishwa na kuanza kutekeleza majukumu yao.