Je, Sonko anajichongea kumshambulia Rais?
Na CHARLES WASONGA
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amewaacha wengi vinywa wazi katika siku za hivi karibuni kutokana na hatua yake ya kumshambulia waziwazi Rais Uhuru Kenyatta hatua ambayo imewashangaza wadadisi wa siasa.
Hii ni kutokana na sababu kwa mapema mwaka huu ni Rais Kenyatta aliyeingilia kati na kumwokoa pale madiwani walipotaka kumwondoa mamlakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye kwa kukwamisha shughuli za serikali ya kaunti ya Nairobi.
Madiwani wakiongozwa wa kiranja wa wachache Peter Imatwok (Diwani wa Makongeni) walitaka kuchukua hatua hiyo baada ya mahakama kuu kumzuia Bw Sonko kuingia afisini hadi kesi ya ufisadi inayomkabili itakaposikilizwa na kukamilishwa.
Gavana Sonko alihusishwa na sakata ya utoaji zabuni ya kima cha Sh345 milioni kwa kampuni kadhaa za kuzua takataka kinyume cha sheria.Rais Kenyatta alizima mpango huo, wa kumwondoa afisini Sonko, ili kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mwingine ikizingatiwa kuwa Gavana huyo hajawahi kuteua Naibu Gavana tangu Polycarp Igathe alipojiuzulu mnamo Januari 2018.
Baadaye kiongozi wa taifa alibuni Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) mnamo Machi 15, 2021 na kuitwika wajibu wa kusimamia utekelezaji wa majukumu manne makuu ya kaunti ya Nairobi, kulingana na mamlaka aliyopewa na Katiba.
Majukumu hayo ni; Afya, Uchukuzi, Mipango na Huduma za Maji na Uzoaji taka.Lakini Sonko hajaridhika na amekuwa akimpiga vita Mkurugenzi Mkuu wa NMS Meja Jenerali Mohammed Badi licha ya kwamba Rais amekuwa akimsihi kila mara afanye kazi na afisa huyo “kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Nairobi”.
Wiki jana, Gavana huyo sasa alimgeukia Rais Kenyatta kwa kuelekezea cheche za shutuma, kupitia mitandao ya kijamii, kuhusiana na shughuli mbalimbali zinazoendeshwa na Serikali ya Kitaifa katika kaunti ya Nairobi.Sonko, ambaye zamani alihudumu kama Seneta wa Nairobi na Mbunge wa Makadara, alikaripia Rais kuhusiana na ubomoaji wa vibanda vilivyojengwa karibu na njia ya reli katika eneobunge la Kibra.
Zoezi hilo linaendeshwa na Shirika la Reli Nchini (KR) kutoa nafasi kwa ukarabati wa reli hiyo ya zamani kutoka Nairobi hadi Kisumu na Malaba.Gavana huyo alidai Rais Kenyatta amegeuka kuwa “kiongozi mbaya asiyejali masilahi ya wananchi wa tabaka la chini.”
“Tunakuheshimu (Rais Kenyatta) lakini hatukuogopi. Tutaongea ukweli bila kujali chochote. Sisemi hivi kwa sababu umenipokonya majukumu makuu ya kaunti. Lakini mahala tumefika sharti tuongee. Tumechoshwa na utawala wako,” akafoka Bw Sonko kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Aliongeza kuwa ikiwa wananchi wataendelea kuteswa na kudhulumiwa, akirejelea ubomoaji uliotekelezwa katika mitaa ya Kariobangi North na Ruai mnamo Aprili mwaka huu, hivyo atakatisha uhusiano wake na Rais.
Siku mbili baadaye, Gavana Sonko alitoa kauli nyingine mitandaoni kuashiria kuwa ameamua kufuata mkondo mwingine za kisiasa wakati huu na hata kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
“Nyakati hubadilika zaidi. Unaweza kuwa na msimamo mmoja leo lakini ukawa na msimamo mwingine tofauti kabisa kesho. Mustakabili wa mtu maishani hubadilika katika mapito ya nyakati. Ni hayo tu kwa sasa,” Sonko akasema kupitia ujumbe katika Facebook.
Katika hali ya kutaka kutanzua maana ya ujumbe wake Bw Sonko aliandamanisha taarifa hiyo na video inayomwonyesha akimsifia Rais Uhuru Kenyatta kiasi cha kutoa kauli kwamba Rais angali na umri mdogo na anapasa kuendelea kuhudumu kama Rais kwa muhula mwingine ili akamilishe miradi yake na juhudi zake za kuunganisha taifa ‘kwa kukomesha siasa za fujo.’
Kulingana na Katiba ya sasa, huu ndio muhula wa mwisho wa Rais Kenyatta kuhudumu kwani ni wake wa pili tangu alipoingia mamlakani kwa mara ya kwanza mnamo 2013. Ametangaza wazi kwamba yu tayari kustaafu 2022.
Isitoshe, Bw Sonko amekuwa akikutana na wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto ishara wazi kwamba ameamua kushabikia mrengo wa Tangatanga ambao unaunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.
Naibu Rais mwenyewe amewahi kukutana na madiwani kadhaa wa Nairobi ambao ni wandani wa Sonko katika makazi yake rasmi ya Karen kando na kwamba madiwani hao wamekuwa wakiandamana na Dkt Ruto katika ziara zake nchini.
Ikumbukwe kuwa kabla ya Naibu Rais kufanya mikutano ya kuchanga fedha katika kaunti ya Nyamira majuma mawili yaliyopita, Gavana Sonko alikutana na wabunge wa kaunti hiyo afisini mwake eneo la Upper Hill.
Wabunge hao walikuwa pamoja na; Vincent Mogaka (Mugirango Magharibi), Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), Shadrack Mose (Kitutu Masaba) ambao ni wandani wa Dkt Ruto na wanachama wa vuguvugu la “Hustler Nation.”
Hata hivyo msemaji wa Sonko Ben Mulwa anasema shutuma ambazo gavana huyo alielekezwa kwa Rais Kenyatta na serikali yake “hazionyeshi kwamba hamheshimu kiongozi wake taifa bali anaendeleza tu mwenendo wake wa tangu zamani wa kupigania masilahi ya wanyonge katika jamii.
Lakini mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anasema shutuma ambazo Sonko alimwekezea Rais Kenyatta zinaashiria kiongozi mwenye machungu baada ya ushawishi wake katika serikali ya kaunti ya Nairobi kuyeyushwa na NMS inayoongozwa na Meja Jenerali Badi.
Kulingana na mchanganuzi huyo hatua hiyo inaweza kumwathiri kisiasa Bw Sonko ikizingatiwa kuwa bado anazongwa na kesi za ufisadi mahakamani.
Kauli hii ni tofauti na yake Bw Martin Andati ambaye anaona ukaidi wa Sonko dhidi ya Rais Kenyatta kama jambo ambalo litamwezesha kujijengea himaya yake kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.