Habari Mseto

Jihadharini na wakora wa siasa, aonya Raila

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM, Bw Raila Odinga amewashauri Wakenya kujihadhari na matapeli wa kisiasa wanaotumia uongo kuingia mamlakani.

Bw Odinga aliyekuwa akihutubia chama cha wafanyabiashara na wataalamu (Nairobi Rotary Club), alisema Kenya inakabiliwa na changamoto tele kama vile ufisadi, ukabila na ukosefu wa ajira, hivyo, inahitaji kiongozi mwenye maono ili kuzitatua.

“Mara nyingi tunaketi chini na kuanza kulalamika kwa hasira na kutafuta mtu wa kulaumu. Baadhi ya wanasiasa wanatumia fursa hiyo kuhadaa wananchi kuwachagua. Lakini baada ya kuchaguliwa wanawaumiza wananchi hao zaidi badala ya kuwasaidia kujikwamua kimaisha,” akasema Bw Odinga.

Kongozi huyo wa ODM alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na Wakenya wote kujenga taifa.

“Mimi si mtakatifu na wala siwezi kudai kuwa nina uwezo wa kukomboa taifa hili au kundi la watu. Mimi ni Mkenya wa kawaida na niko tayari kushirikiana na Wakenya wenzangu; maskini kwa matajiri, wanaume kwa wanawake au wazee kwa vijana ili kujenga taifa,” akasema.

Bw Odinga alionekana kumshambulia Naibu wa Rais, Dkt William Ruto ambaye amekuwa akidai kuwa kiongozi huyo wa ODM, Rais Uhuru Kenyatta na Seneta wa Baringo Gideon Moi ni ‘wana wa wafalme’ ambao hawataki kuona mtoto wa maskini akiwa rais wa nchi hii.

Naibu wa Rais amekuwa akiwataka Wakenya walala-hoi (hasla) kukataa mabwanyenye katika Uchaguzi Mkuu ujao. Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa Wakenya walalahoi wakiongozwa naye, ndio watakaobuni serikali ijayo.

Lakini viongozi wa dini na wanasiasa wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakimshutumu vikali Naibu Rais kwa kuwagonganisha Wakenya wa mapato ya chini dhidi ya mabwanyenye.

Kulingana nao, hatua ya kuchochea maskini dhidi ya matajiri huenda ikazua ghasia kama zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Bw Odinga amekuwa akikutana na makundi mbalimbali katika juhudi za kuupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI). Jumatatu, alikutana na viongozi kutoka maeneo ya wafugaji ambapo aliwahimiza kuunga mkono BBI.