Habari MsetoSiasa

Juhudi za kumng'oa Spika Muturi, Duale na Mbadi zaanza

September 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na WAANDISHI WETU

WABUNGE waliowakaidi Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kuhusu Mswada wa Fedha wa 2018, sasa wanapanga kuanzisha juhudi za kuwang’oa mamlakani viongozi wao bungeni.

Wabunge hao wa pande tofauti za kisiasa wamekasirishwa na jinsi mswada huo ulivyopitishwa kimabavu katika Bunge wiki iliyopita, na sasa wanataka viongozi akiwemo Spika Justin Muturi, Kiongozi wa Wengi Aden Duale, na mwenzake wa wachache John Mbadi waadhibiwe.

Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter, Jumapili alisema haifai bunge lote kukashifiwa kwa matukio yaliyoshuhudiwa wiki iliyopita, bali lawama inafaa ielekezwe kwa viongozi wao ambao alisema walivuruga shughuli hasa wakati wa kupitishwa kwa mswada uliohusu ongezeko la ushuru wa bidhaa za mafuta.

Wiki iliyopita, Bw Muturi aliwaambia wabunge hao waache kumlaumu kwani wao ndio walikosa kupanga mikakati yao ipasavyo ili kuzuia mswada huo kupitishwa.

Mbunge wa Mwingi Magharibi Charles Nguna, alidai wakuu bungeni waliwanyanyasa wabunge kwa kuwaibia ushindi wao katika kura zilizopigwa kwenye kikao maalum bungeni ili kupitisha mswada huo.

Wabunge wengine waliapa kwenda mahakamani ili mswada huo ulioidhinishwa kuwa sheria utupiliwe mbali, huku Chama cha Thirdway Alliance kikitoa wito kwa wabunge wanaodai kusimama na wananchi waungane kubadilisha sheria hiyo bungeni.

Wabunge Justus Murunga (Matungu), Ayub Savula (Lugari) na Mbunge Maalum Godfrey Osotsi ambao wote ni wa Chama cha Amani National Congress, walisema hawatakaa kitako na kutazama Wakenya wakiumia.

Kulingana na sheria za Bunge, baada ya mswada kupitishwa bungeni na kutiwa sahihi na Rais, unaweza tu kujereshwa bungeni tena baada ya miezi sita. Ni wakati muda huo ambapo mbunge anaweza kupenyeza marekebisho ambayo wangetaka yafanyiwe sheria husika, kwa kutayarisha mswada mpya unaojumuisha masuala yanayolengwa.

Ripoti ya VALENTINE OBARA, BONIFACE MWANIKI, SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA