Habari Mseto

Polisi wasema hawatawashtaki wanahabari wa NTV

February 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Kutoka kulia: Wanahabari wa runinga ya NTV Linus Kaikai, Larry Madowo na Ken Mijungu watabasamu ofisini katika jumba la Nation Centre, Kimathi Street, Nairobi. Picha/ Maktaba

Na RICHARD MUNGUTI

Kwa Muhtasari:

  • Polisi hawatawachukulia hatua yoyote wanahabari Linus Kaikai, Larry Madowo na Ken Mijungu
  • Hakuna haja kwa walalamishi kuendelea kuishi na hofu ya kutiwa nguvuni kwa kuwa hakufanya kosa lolote
  • Jambo ambalo lilifanya polisi kuwasaka ni uapisho wa Bw Raila Odinga

POLISI  waliamriwa Jumatatu na Mahakama Kuu  wasiwasumbue wanahabari wa shirika la Nation Media Group.

Pamoja na hayo polisi waliambia korti hawana mpango wa kuwashtaki wanahabari watatu wa shirika hilo.

Wakili wa serikali alimweleza Jaji Luka Kimaru  kuwa polisi hawatawachukulia hatua yoyote Mabw Linus Kaikai, Larry Madowo na Ken Mijungu, wote wa runinga ya NTV.

“Hakuna haja kwa walalamishi kuendelea kuishi na hofu ya kutiwa nguvuni. Hakuna kosa lolote walilofanya wanahabari hawa. Polisi wamesema hawana haja ya kuwafungulia mashtaka,” Jaji Kimaru alifahamishwa na wakili wa serikali.

Wiki iliyopita wanahabari hao walikimbia mahakamani na kuomba mahakama kutoa agizo kwa polisi wasiwakamate.

 

Wasiwasi

Hii ni baada ya watatu hao kushikwa na wasiwasi kuwa wangetiwa mbaroni kwenye msako uliokuwa ukiendelezwa dhidi  ya watu waliohusika katika hafla ya kuapishwa kwa Raila Odinga kuwa “rais wa wananchi”.

Walalamishi hao kupitia kwa wakili wao walisema jambo ambalo lilifanya polisi kuwasaka ni uapisho wa Bw Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018 na “ matukio kuhusu suala hilo yangali moto na vyombo vya habari vinaendelea kuyaangazia.”

Wanahabari hao waliomba korti itoe agizo polisi wasiwashike na kuwashtaki kwa vile suala la uapisho wa Bw Odinga ni  tukio linaloendelea kujadiliwa katika hafla mbalimbali na “ wanahabari lazima wapeperushe taarifa za matukio kuhusu shughuli hiyo.”

Walipewa dhamana ya Sh100,000 ili polisi wasiwazuilie katika kituo chochote cha polisi.

Kesi hiyo itatajwa tena baada ya wiki mbili.