Kampuni ya mikopo yajitetea ikizidi kulaumiwa kwa kupotosha wateja
KAMPUNI ya kutoa mikopo ya kununua magari, Boda Boda na Tuk Tuk nchini, Mogo Kenya, imeelewana na Mamlaka ya Ushindani Nchini (CAK) kuhusu tuhuma kwamba iliwapunja wateja wake kwa kuwalazimisha kulipa mikopo ya juu kinyume na masharti yaliyowekwa.
Kupitia taarifa iliyotuma kwa vyombo vya habari Ijumaa, Oktoba 4, 2024, kampuni ilisema kuwa hali hiyo ilitokea kufuatia mabadiliko katika viwango vya thamani ya dola ya Amerika dhidi ya Shilingi ya Kenya tangu 2022.
Mogo Kenya ilitoa mikopo kwa chini ya asilimia 15 ya wateja wake kwa kutumia dola ya Amerika inayovutia riba ya chini.
“Kwa bahati mbaya kutokana na mabadiliko katika thamani ya sarafu hiyo ya kigeni, kiwango cha mkopo ambao wateja kama hao walilipa kiliongezeka. Malalamishi yalipoibuliwa kupitia CAK, Mogo iliamua kufikia makubaliano na mamlaka hiyo na walalamishi husika,” Mogo ikasema.
“Ni muhimu kutaja kwamba makubaliano hayo yanaashiria nia njema kutoka kwa pande husika na sio kwamba Mogo imetozwa faini kwa makosa ya kutoa mikopo kwa sarafu ya dola kwani hatua hiyo ni halali kwa misingi ya sheria ambayo kampuni hiyo huzingatia nchini Kenya.”
Kampuni hiyo inasema kuwa kutokana na hitilafu kama hiyo, imesitisha utoaji wa mikopo kwa sarafu ya dola kuanzia Mei 2024.
Mogo Kenya, ambayo ni tawi la Mogo Auto Limited, imetoa ufafanuzi huo kufuatia ripoti kwamba imetozwa faini kima cha Sh10.85 milioni na mamlaka ya CAK kwa kosa la kutekeleza masharti potovu ya mikopo.
Kulingana na ripoti hiyo iliyochapishwa katika gazeti la “Business Daily”, kampuni hiyo pia iliamriwa kurejesha zaidi ya Sh340,000 kwa wateja watatu waliolipa zaidi ya pesa walizohitajika kulipa kwa mujibu wa masharti asilia.
Kwenye taarifa yake, Mogo Kenya imekariri kujitolea kwake kuendelea kutoka mikopo ya gharama nafuu kwa ununuzi wa magari yaliyotumika, pikipiki za boda boda na Tuk Tuk kwa ajili ya kupiga jeki sekta ya uchukuzi nchini Kenya.