Kanze Dena ateuliwa Naibu Msemaji wa Ikulu
Na LEONARD ONYANGO
RAIS Uhuru Kenyatta amefanyia mabadiliko Kitengo cha Mawasiliano ya Rais (PSCU) Jumanne huku mtangazaji wa runinga ya Citizen Kanze Dena akiteuliwa kuwa naibu wa Msemaji wa Rais.
Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Wafanyakazi wa Kitengo cha PSCU Nzioka Waita, Bi Dena, 39, atakuwa naibu wa Manoah Esipisu na atasimamia mitandao ya kijamii, utafiti, kudumisha sifa njema ya Ikulu na kusimamia mikutano ya wanahabari.
“Bi Dena atasimamia mitandao ya kijamii, habari na utafiti. Bi Dena ana ujuzi wa uanahabari na atatakiwa kudumisha uhusiano mwema na vyombo vya habari kutoa taarifa sahihi kuhusiana na Miradi Mikuu Minne ya rais,” akasema Bw Waita.
Rais Kenyatta pia alimteua Bi Munira Mohamed, 40, kuwa Naibu wa Mkuu wa Kitengo cha Maktaba ya Rais.
Bi Mohamed atahakikisha kuwa anahifadhi kazi, picha, video na hotuba za marais ambao wamewahi kuongoza kenya. “Rais aliidhinisha kubuniwa kwa Maktaba ya Rais, Kituo cha Maonyesho ya Makavazi.
Maktaba hiyo itakuwa na masuala yanayohusiana na hayati Mzee Jomo Kenyatta, marais wastaafu Daniel Toroitich arap Moi na Mwai Emilio Kibaki,” akasema Bw Waita.
Bi Mohamed ataongoza kikosi kitakachofanya kazi ya kuandaa maktaba hiyo na kituo cha maonyesho.
“Bi Mohamed atashirikiana na familia za viongozi hao watatu na Idara ya Utamaduni kubaini hotuba, stakabadhi, vitabu, michoro na mambo mengineyo yanayofaa kuhifadhiwa katika maktaba,” akaongezea.
Bw Esipisu ataendelea kuwa msimamizi wa PSCU na msemaji wa rais.
“Rais Kenyatta anaamini kuwa wanawake hao wawili watakuwa wa manufaa makubwa katika kitengo cha PSCU,” akasema Bw Waita.