Habari MsetoSiasa

Karua bado aamini alimbwaga Waiguru, akata rufaa tena

June 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na JOSEPH WANGUI

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua, amewasilisha rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali kesi yake ya kupinga ushindi wa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru.

Kwenye ilani ya rufaa, Bi Karua, pamoja na aliyekuwa mbunge wa Kirinyaga ya Kati, Bw Joseph Gitari, walisema wanapinga uamuzi wote uliotolewa na Jaji Lucy Gitari mnamo Juni 14, 2018 katika Mahakama Kuu mjini Kerugoya.

“Mlalamishi, Martha Karua, kwa kukosa kuridhishwa na uamuzi na agizo la Jaji Gitari, anapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi wote,” inasema ilani kwa washtakiwa wote wanne katika kesi yake.

Baada ya jaji kutupilia mbali kesi yake, Bi Karua aliambia wafuasi wake kwamba angepinga uamuzi huo katika mahakama ya rufaa.

Alitaja Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), msimamizi wa uchaguzi katika kaunti hiyo Seki Lempaka na Gavana Waiguru pamoja na naibu wake Peter Ndambiri kama washtakiwa katika kesi hiyo.

Bi Karua anataka ushindi wa Gavana Waiguru ubatilishwe akidai hakushinda kwa njia huru na ya haki kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8 2017.

Kwenye uchaguzi huo, Gavana Waiguru alipata kura 161,373 naye Bi Karua alipata kura 122,091.