Kaunti Ukambani ambayo ina wafanyakazi wengi wa kike kuliko wa kiume
SERIKALI ya Kaunti ya Makueni imeajiri idadi kubwa ya wanawake kuzidi wanaume, maseneta walijulishwa Jumatatu, Agosti 19, 2024.
Gavana wa kaunti hiyo Mutula Kilonzo Junior, aliyefika mbele ya wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Uwiano, Usawa na Utangamano wa Kikanda wakiongozwa na Seneta wa Marsabit Mohamed Chute, alisema asilimia 61 wa wafanyakazi wa umma katika serikali yake wanatoka jinsia ya kike.
“Kati ya wafanyakazi 3, 815 walioajiriwa na serikali yangu, 2, 311 ni wanawake ilhali 1, 504 ni wanaume. Hii ina maana kuwa wanawake wanashikilia asilimia 61 za nafasi za ajira huku wanaume wakishikilia asilimia 39 za nafasi,” Bw Kilonzo Junior akasema.
“Aidha, miongoni mwa maafisa hao 91 ni watu wanaoishi na ulemavu wanaowakilisha asilimia 2.4 ya idadi jumla ya wafanyakazi katika serikali ya kaunti ya Makueni,” akaongeza.
Kamati hiyo imekuwa ikiendesha uchunguzi kuhusu uajiri katika serikali za kaunti kwa kuzingatia vigezo vya jinsia, watu wanaoishi na ulemavu, umri na uwakilishi wa kikabila.
Gavana Kilonzo Junior pia aliiambia kamati hiyo kwamba idadi ya wafanyakazi kutoka jamii zingine walioajiriwa katika kaunti ya Makueni ni 281 inayowakilisha asilimia 8.4 ya idadi jumla ya wafanyakazi.
Kipengele cha 232 cha Katiba kinasema kuwa usawa unafaa kuzingatiwa kati ya wanaume na wanawake katika ngazi zote za utumishi wa umma.
Aidha, Katiba inahitaji kwamba serikali za kaunti na serikali ya kitaifa kutenga nafasi stahiki za ajira kwa watu wanaoishi na aina mbalimbali za ulemavu katika ngazi zote za utumishi wa umma.
Angalau asilimia tano ya nafasi hizo zinafaa kutengewa watu wa tabaka hilo.
Stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Seneta Chute na Bw Kilonzo zinaonyesha kuwa watu kutoka jamii ya Akamba ndio wanashikilia asilimia 92.63 za idadi jumla ya nafasi za ajira ambayo ni sawa na nafasi 3,534.
Jamii ya Agikuyu inashikilia nafasi ya pili kwa kushikilia nafasi 90 au asimilia 2.36 ya nafasi zote, jamii ya Ameru (nafasi 36), Wakisii (32), Waluhya (26), Waluo (24) huku watu kutoka jamii ya Wakalenjin wakishikilia nafasi 22 katika serikali ya kaunti ya Makueni.
Wengine ni; Waembu wanaoshikilia nafasi 15, Wataita (8), Wamiji Kenda (6), Wambeere (4), Wamaasai (3), Wasomali (2), watu kutoka jamii za Swahili Shirazi (2) sawa na Watharaka.
Kila moja ya jamii za Ajurana, Waborana, Wadegodia, Wakuria, Wapokomo, Wasekuye, Wataveta, Wateso Sakuye, Wataveta, Wateso na Waturkana zinawakilishwa na mtu mmoja katika serikali ya Kaunti ya Makueni.
-Imetafsiriwa na CHARLES WASONGA