Habari Mseto

Kazi ya uchifu yaepukwa Lamu kutokana na mauaji

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KALUME KAZUNGU na MISHI GONGO

WAKAZI wa vijiji vya Kaunti ya Lamu ambavyo vimekuwa vikishuhudia mauaji ya mara kwa mara ya maafisa wa usalama wanaishi kwa hofu tele, kwani sasa hakuna wakazi wanaotaka kujaza nafasi za machifu zilizoachwa wazi.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na visa vya mauaji ya machifu, manaibu wao, wanachama wa makundi ya nyumba kumi na polisi katika vijiji vilivyo Tchundwa, Mbwajumwali na Myabogi.

Imefichuka kuwa, wakazi wa Lamu wamesusia kuwasilisha maombi ya kazi za machifu licha ya serikali kutangaza nafasi hizo kuwa wazi kwa kipindi cha miezi saba sasa.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alikiri kwamba serikali imepata changamoto kubwa kujaza nafasi za machifu tangu chifu na naibu wake kuuawa kinyama eneo hilo mwaka uliopita.

“Tumetangaza nafasi hizi lakini hakuna mtu anayejitokeza kufanya kazi hizo katika maeneo hayo. Mbali na machifu kuogopa kuajiriwa eneo hilo, huenda hata polisi wetu pia wakaanza kughairi kupelekwa kuhudumia maeneo husika,” akasema.

Mnamo Disemba 11, 2019, chifu wa lokesheni ya Mbwajumwali Mohamed Haji Famau, 45 na Naibu wake ambaye ni wa lokesheni ndogo ya Myabogi, Malik Athman Shee, 43 waliuawa wakati watu wawili waliovalia buibui na kufunika nyuso zao kwa ninja walipowavamia ofisini mwao mjini Mbwajumwali na kuwakatakata kwa mapanga kabla ya kutoroka.

Mnamo Juni 8 mwaka huu ambapo afisa wa polisi wa cheo cha konstebo, Bw Rodgers Odhiambo aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana akiwa mjini Tchundwa, Lamu Mashariki.

Oktoba mwaka uliopita, Konstebo wa Polisi aliyehudumu kwenye kituo hicho hicho cha Tchundwa, Hesbon Okemwa Anunda pia aliuawa kwa kukatwakatwa kwa panga na watu wasiojulikana.

Aprili mwaka huo, Afisa wa Nyumba Kumi ambaye pia alikuwa mfanyikazi wa kujitolea wa Shirika la Kenya Red Cross, Bi Amina Bakari, 30, aliuawa kwa kukatwakatwa kwa panga na watu wasiojulikana wakati akifunga duka lake kijijini Mbwajumwali.

Mnamo Juni, 2016, chifu mkuu wa Mbwajumwali, Mohamed Shee, 50 aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana wakati akielekea kazini majira ya saa tatu asubuhi.

Bw Macharia alisema matukio hayo yameingiza wakazi wasiwasi. Alisema kufikia sasa serikali imetoa matangazo mara tatu kwenye maeneo husika ya kuwataka wakazi kuwasilisha maombi ili waajiriwe machifu na manaibu wao lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza.

“Wengi wanachukulia kuwa chifu au naibu wa chifu maeneo hayo ni sawa na kujitia kitanzi. Ni jambo la kusikitisha,” akasema Bw Macharia.

Kamishna huyo hata hivyo aliwahimiza wananchi kutoogopa na badala yake kujitokeza kujaza nafasi hizo kwani serikali imefanya mikakati kabambe kuhakikisha usalama wa maafisa wa utawala eneo hilo unadhibitiwa vilivyo.

“Machifu wamekuwa wakiuawa kiholela kwenye maeneo husika. Siku za hivi karibuni wahalifu pia wamewageukia polisi na kuwaua,” akasema Bw Macharia.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo walikiri kuwa katu hawawezi kuchukua kazi hizo za machifu na manaibu wao, ikizingatiwa kuwa maafisa wa utawala eneo hilo wamekuwa wakilengwa na magenge hatari.