Habari Mseto

KDF bandia kortini kwa kuibia mpenziwe Sh36,000

March 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MWASHI aliyejifanya kuwa afisa wa Jeshi (KDF) na kumwibia mpenzi wake Sh36,000 na simu ya rununu alishtakiwa Jumatano.

Lakini Bw Dennis Makori Isaboke aligeuza maneno alipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot na kufichua kwamba “walikosana na mpenzi wake kisha akamweleza kwamba atalilia kwa choo ndipo ajue majuto ni mjukuu.”

Bw Isaboke alimweleza Bw Cheruiyot akiomba aachiliwe kwa dhamana: “Naomba hii mahakama iniwie radhi kwa vile nilitishwa na mlalamishi katika hii kesi kwamba nitajuta kwa kutofautiana naye. Bi Lydia Moraa Onchwangi ni mpenzi wangu. Tumekuwa tukichumbiana lakini tulipokosana alinitisha akinieleza nitaona cha mtema kuni.”

Bw Isaboke alimweleza hakimu kwamba alifikiria Bi Onchwangi alikuwa anamtania kumbe alikuwa “ akimaanisha atanitoa jasho kweli kweli.”

Mshtakiwa aliomba korti imwachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu cha pesa kwa vile mimi “ ni mjenzi wa nyumba na sina mapato ya juu.”

Mshtakiwa huyo aliendelea kueleza mahakama kwamba ameshangazwa na kutimizwa kwa vitisho hivyo na Lydia ambaye wamekuwa marafiki kwa muda mrefu.

“ Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana ndipo niendelee kumsaidia mama yangu mkongwe pamoja na ndugu zangu wanaosoma shule ya Sekondari,” alisema Bw Isaboke.

Kiongozi wa mashtaka Bi Cynthia Opiyo hakupinga ombi la kuachiliwa mshtakiwa kwa dhamana.

“Dhamana ni haki ya mshtakiwa. Sipingi akiachiliwa. Uchunguzi umekamilishwa na nitampa mshtakiwa nakala za ushahidi,” alisema Bi Opiyo.

Mshtakiwa alikabiliwa na mashtaka matano ya wizi wa simu za rununu mbili aina ya Infinix Hot 5 katika hospitali kuu ya Kenyatta (KNH). Pia alijifanya afisa wa mamlaka ya bandari na kumwibia Migoro Nyakundi Abela simu aina ya Infinix.