KeMU kuuza jengo lake ili kujiimarisha kifedha
Na OUMA WANZALA
CHUO Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) kimetangaza hatua ya kuuza mojawapo ya majengo yake jijini Nairobi, katika mkakati wa kupata fedha za kutosha kuendeshea shughuli zake.
Hatua hiyo inaashiria mgogoro wa kifedha ambao unavikumba vyuo vikuu kadhaa vya kibinafsi nchini kutokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaosoma kwa mfumo wa kujifadhili.
Kwa sasa, chuo hicho kimetangaza kuuza jengo kubwa la KeMU Hub, lililo katika Barabara ya Koinange, jijini Nairobi. Jengo hilo huwa muhimu, hasa katika shughuli zake za kimasomo.
Kwenye barua kwa Meneja wa Uuzaji katika Benki ya Co-operative, Bi Jacqueline Waithaka mnamo Machi 14, Naibu Chansela katika chuo hicho Prof Oduor Okoth anasema kwamba Baraza Kuu la Usimamizi wa Chuo limepitisha uuzaji wake.
Prof Okoth alisema kwamba hatua hiyo imepelekewa na hali mbaya ya kifedha ambayo inaikabili taasisi hiyo.
“Ni uamuzi wetu kwamba uuzaji wa jengo hilo utatupa kiasi cha fedha tunachohitaji ili kulainisha shughuli na utendakazi wa taasisi hii. Baada ya uuzaji wake, tutatumia sehemu ya fedha hizo kulipia mkopo wa Sh135 milioni ambazo tulichukua kutoka kwa benki yenu mnamo Juni 2017.
Fedha zitakazobaki tutalipia madeni yetu kwa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), malimbikizi ya wahadhiri kati ya asasi zingine,” ikasema barua hiyo.
Aidha, alisema kuwa jengo hilo ni mojawapo ya mali ambayo walitumia ili kupata mkopo wa Sh1.7 bilioni.
Na ikiwa jengo hilo halitamaliza kugharamia kiasi hicho, taasisi hiyo inapanga kuuza jengo la KeMU Towers ili kumalizia kulipa mkopo huo.
Mnamo Januari mwaka huu, Tume ya Elimu ya Juu Kenya (CUE) iliagiza ukaguzi wa katika chuo hicho na Chuo cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).
Kwenye barua iliyotiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i, barua hiyo ilipendekeza taasisi hizo mbili kupewa kipindi cha mwaka mmoja kulainisha shughuli zao.
Barua ilionya kwamba huenda vikanyang’anywa vibali vyao vya kuendesha shughuli zao, ikiwa hazingetimiza kanuni hizo.
Vyuo kadhaa vilikuwa vimetumia mabilioni ya fedha kununulia majengo katika miji mikuu ili kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi ambao wamekuwa wakiongezeka.
Baadhi vilibuni mabewa mengi katika miji mbalimbali nchini. Hata hivyo, hilo limegeuka, baada ya CUE kuweka kanuni kali katika ufunguzi wa mabewa hayo.