Kibra na Mombasa maeneo hatari kwa ueneaji wa corona
VALENTINE OBARA na WACHIRA MWANGI
BANDARI ya Mombasa na mtaa wa Kibra ulio Kaunti ya Nairobi, ni miongoni mwa maeneo ambayo yamo hatarini zaidi kwa ueneaji virusi vya corona.
Waziri Msaidizi wa Afya, Bi Mercy Mwangangi jana alisema maeneo hayo, pamoja na Kaunti za Siaya na Mandera yatapewa kipaumbele wakati wa shughuli ya kuchunguza watu kwa wingi kama wameambukizwa virusi hivyo.
Wakati huo huo, imebainika kwamba visa vya mizozo ya kinyumbani vimeongezeka sana katika kipindi hiki ambapo watu wengi wako nyumbani na familia zao.
“Huu si wakati wa kupigana. Vita pekee ambavyo tunafaa kujihusisha navyo ni dhidi ya janga la corona,” akasema Dkt Mwangangi.
Inaaminika mtaa wa Kibra ulitajwa kwa sababu ya idadi kubwa ya watu wanaoishi eneo hilo ambao husongamana wakati mwingi.
Kwingineko, Chama cha Makuli (DWU) awali kilitoa makataa ya siku tatu kwa Halmashauri ya Kusimamia Bandari (KPA) kutelekeza mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, la sivyo kiitishe mgomo.
Kwenye kikao na wanahabari jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Simon Sang’, alisema kufikia sasa thuluthi moja ya wale waliothibitishwa kuambukizwa virusi Mombasa wanatoka katika eneo la bandari.
Hivyo, aliziomba Serikali ya Kitaifa na zile za kaunti kuwalinda wafanyakazi hao dhidi ya kuambukizwa. Alisema zinapaswa kuchukulia malalamishi yao kwa uzito.
Hata hivyo, chama kinataka shughuli za haraka kuanzishwa kuwakagua zaidi ya maakuli 7,000 ikiwa wameambukizwa kufuatia kifo cha wafanyakazi wawili kwa muda wa wiki moja iliyopita kutokana na virusi hivyo.