Habari Mseto

Kizaazaa muuaji wa marehemu kujitokeza mazishini

December 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

Kizaazaa kilitibuka katika makaburi ya Wanyororo eneo la Bahati, kaunti ya Nakuru siku ya Alhamisi wakati wa mazishi ya mwanaume wa umri wa miaka 33 aliyeuawa juma lililopita. 

Kivangaito hicho kilitokea wakati baadhi ya jamaa wake walipinga kuzikwa kwake kabla ya polisi kutoa habari kuhusu kuachiliwa kwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo aliyeachiliwa muda mfupi baada ya kukamatwa.

Kulingana na jamaa hao, marehemu Edward Mwangi alipatikana amefariki mnamo tarehe 3 Desemba shambani katika eneo hilo huku mwili make ukiwa umevuja damu baada ya kudungwa kwa kisu.

Kaburi lililoandaliwa kwa mazishi. Picha/ Maggy Wanja

Chifu wa eneo hilo alipofika katika eneo ambalo marehemu alikuwa ameuawa, aliwauliza wakazi kama kuna yeyote aliyekuwa na habari kuhusu kilichotokea.

“Mwanaume mmoja alijitokeza akiwa na kisu mkononi na kusema kuwa ndiye alimuua Mwangi,” alisema Bw Charles Mucheru ambaye ni mpwa wa mwendazake.

Baada ya kukamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi, jamaa wa mwendazake wanasema kuwa mshukiwa huyo aliachiliwa bila ya hatua yoyote kuchukuliwa.

“Maafisa wa polisi waliokuwa katika kituo hicho cha polisi hawakutukabidhi nambari ya OB kuonyesha kwamba kisa hicha kilikuwa kimeripotiwa. Hii ilitushangaza sana,” aliongeza Be Mucheru.

Wanakijiji walikusanyika ka mazishi lakini yakaingia mzozo baina ya polisi na familia ya mwendazake. Picha/ Maggy Wanja

Wakati wa mazishi yaliyopangiwa kufanyika siku ya Alhamisi , baadhi ya jamaa wa mwendazake, akiwemo mkewe marehemu walipinga kuzikwa kwake kabla ya maafisa wa polisi kuwapa majibu kuhusu kuachiliwa kwa mshukiwa huyo.

Mkewe marehemu pamoja na mpwa wa marehemu waliingia ndani ya kaburi lililochimbwa kupinga mazishi hayo na kusababisha mvutano kati ya pande hizo mbili  kwa zaidi ya saa tatu.

Upande mwingine wa jamii hiyo ulitaka mwili wa mwendazake kuzikwa kabla ya kufuatiliwa kwa kesi hiyo.

Mwendazake ambaye alikuwa mchezaji kandanda wa timu ya eneo hio ijulikabayo kama Greenbelt alikuwa baba ya watoto wawili.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, usiku wa kisa hicho, marehemu alihusika katika vita kutokana na mzozo wa kimapenzi.

Hatimaye mwili huo ulizikwa licha ya pingamizi kali.