Habari Mseto

KNBS yajitetea kuhusu Sh18 bilioni za sensa

January 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

WIZARA ya Fedha pamoja na Taasisi ya Unakili wa Takwimu Nchini (KNBS) Jumatano zimetetea bajeti ya Sh18.5 bilioni zitakazotumika kufanya sensa mwaka huu, zikisema kuwa teknolojia itakayotumiwa, muda wa mafunzo na idadi ya wafanyakazi  ndiyo sababu.

Waziri Henry Rotich jana alisema kuwa kiwango hicho cha pesa ambacho wizara yake ilitenga kwa zoezi hilo si cha juu namna serikali imekuwa ikikosolewa, akisema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa hesabu ya watu mwaka huu haiingiwi na doa.

Wakati huohuo, Bw Rotich pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa KNBS Zachary Mwangi aliwatahadharisha Wakenya kuhusu matapeli ambao wameanza kutumia mitandao ya kijamii kudai kuwa wanapeana kazi zinazohusiana na sensa, wakisema tangazo hilo litatolewa na serikali tu.

“Wacha nitahadharishe umma kuhusu kuhadaiwa na matapeli ambao wamejiandaa kuwadanganya kwa ahadi za kazi. Serikali haitawahitaji kulipa pesa zozote ili kupata kazi na pia KNBS na wizara yetu zina tovuti rasmi ambapo jumbe rasmi huchapishwa,” akasema Bw Rotich. “Shughuli za kuajiri watu watakaofanya kazi hiyo zitaanza Juni.

Kutoka kushoto: Mwenyekiti wa muungano wa wahariri Churchill Otieno, Waziri wa Fedha Henry Rotich na katibu katika wizara hiyo Dkt Julius Muia katika kikao na wanahabari Jijini Nairobi Januari 23. Picha/ Peter Mburu

Wakizungumza wakati wa kikao na waandishi wa habari, Bw Rotich na Bw Mwangi walisema kuwa kwa mara ya kwanza, Kenya itafanya sense kwa njia za kiteknolojia, bila kutumia karatasi.

Vilevile, walisema kuwa hali hiyo itafanya matokeo ya sense kutolewa mapema kuliko sense za mbeleni nchini, serikali ikitarajia kuwa kufikia Desemba, matokeo yatakuwa yametolewa.

“Teknolojia itapunguza muda ambao hutumiwa kutoa matokeo ya sense. Tutawaajiri watu 135,000 kuhesabu, watu 27,000 kama wasimamizi na watu 2,700 kushughulikia mitambo (ICT),” akasema Bw Mwangi.

Bw Mwangi alisema kuwa vifaa 164,000 vya kidijitali ambavyo serikali itanunua kutekeleza sensa baadaye vitapelekwa mashuleni kutumiwa katika masomo.

Waziri wa Fedha Henry Rotich. Picha/ Peter Mburu

“Baada ya sensa kukamilika, vitatolewa habari na kuwekwa habari za masomo kasha zipelekwe katika shule watoto wakatumie. Aidha, tunatumia vyuo vikuu vya Moi na JKUAT kutusambazia vifaa hivyo kama mbinu ya kuinua taasisi zetu za elimu,” akasema mkurugenzi huyo wa KNBS.

Hadi kufikiia sasa, shirika la KNBS limefanya mpango wa jinsi zoezi hilo litaendeshwa katika kaunti 38 na zilizosalia zinatarajiwa kukamilika kufikia Aprili.

Waziri Rotich alisema kuwa wanatarajia kufanya vikao na wanasiasa pia ili kuwahamasisha kuhusu masuala ya sensa, kuepuka hali ambapo siasa zitaingizwa katika zoezi hilo.

Alisema kuwa baada ya hesabu ya mwaka huu kufanywa kidijitali, zitakazofuata zitakuwa rahisi na za gharama ya chini, kwani kitu kikubwa kitakuwa tu kufanyia mabadiliko habari zitakazokuwa.

“Aidha, tunataka sensa ya mwaka huu kuwa na mambo mageni kama rekodi ya watu wenye ulemavu na wengine wenye mahitaji spesheli, ili watengewe nafasi na rasilimali zao ipasavyo,” akasema waziri huyo.