Knut yataka pensheni ilipwe na TSC kuepuka walimu kuzungushwa na Wizara ya Fedha
CHAMA cha Walimu Nchini (KNUT) sasa kinataka mabadiliko yafanyiwe Sheria ya Pensheni ili kuzuia walimu wanaostaafu kuchelewa kulipwa kiinua mgongo chao.
Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Kitaifa wa Kike wa KNUT Mercy Ndungú walimu ambao hustaafu huteseka sana kwa kukosa kulipwa pensheni zao kwa wakati.
Bi Ndungú alisema Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC) inastahili kupewa mamlaka ya kulipa pensheni moja kwa moja badala ya Hazina Kuu ya Fedha.
“Kuzuia kuchelewa huko, TSC inastahili kupewa mamlaka kushughulikia pensheni kwa walimu wastaafu,” akasema Bi Ndungú ambaye alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa kila mwaka tawi la Kirinyaga.
Afisa huyo alilalamika kuwa inachukua zaidi ya miaka mitatu kwa walimu kupokea pensheni zao baada ya kustaafu. Alisema ni masikitiko makubwa kuwa baadhi ya walimu hufa hata kabla ya kunufaikia malipo yao ya uzeeni.
“Hi sii haki hata kidogo, tunawataka walimu wote wapate pesa zao baada ya tu kustaafu ili waanzishe biashara au miradi ya kuwainua kimapato,” akasema.
Pia aliwataka wanasiasa wakome kuingiza siasa kwenye mchakato wa kuwaajiri walimu.
“Tumeona hali ambapo wanasiasa wamekuwa wakitoa barua za ajira kwa wafuasi wao kwenye mikutano ya umma na makanisa. Hili ni jambo ambalo halikubaliki na ni vyema iwapo taaluma ya ualimu itaheshimiwa,” akasema.
“Kama wanasiasa ndio wanatoa barua za ajira, basi taaluma ya ualimu inaelekea wapi?” akauliza.
Aliongeza kuwa Knut inawajibika na itahakikisha kuwa walimu wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri, itawatetea na kuhakikisha kuwa serikali inaheshemu mikataba iliyotia saini nao.