Kongamano kuhusu tabia-nchi kufanyika Makueni
Na Benson Matheka
Kongamano la ugatuzi mwaka huu litafanyika mjini Wote, Kaunti ya Makueni kati ya Aprili 20 na 23 mwaka huu, baraza la magavana (COG) limetangaza.
Baraza hilo lilisema kwamba mada ya kongamano la mwaka huu ni kuhusu mabadiliko ya tabianchi, hasa wajibu wa serikali za kaunti katika mabadiliko hayo.
“Hatua ya kuangazia mabadiliko ya tabianchi imesababishwa na madhara yake kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Kenya. Hii imesababisha mazingira duni ya kuishi katika baadhi ya maeneo, mafuriko, ukame, utoaji wa taka kutoka viwandani usiodhibitiwa na kuongezeka kwa gharama ya matitabu,” COG ilisema kwenye taarifa.
Kulingana na baraza hilo, serikali za kaunti na ya taifa zina jukumu la kuhakikisha kwamba raia wana chakula cha kutosha, upatikanaji wa huduma bora za afya kwa gharama nafuu, nafasi za kazi zimebuniwa, na serikali na sekta ya kibinafsi zimedhibiti utoaji wa taka.
“Kongamano hili litakuwa muhimu kwa serikali za kaunti, kimaeneo, kikanda na hata kimataifa kujadili jukumu lao na jinsi zinavyoweza kubadilisha athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii,” ilieleza COG.
Waandalizi wa kongamano hilo wanasema kwamba kuna haja ya kuchukua hatua kuweka sheria, kufadhili na kuidhinisha mikakati ya kupunguza hatari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Mada za makongamano sita yaliyotangulia ziliangazia safari na ufanisi wa ugatuzi, jukumu la serikali za kaunti katika utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za serikali miongoni mwa masuala mengine.
Kongamano la sita liliandaliwa kaunti ya Kirinyaga. COG ilisema kwamba lengo kuu la kongamano la saba linanuiwa kupatia serikali za kaunti uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Itakuwa jukwaa la serikali na sekta ya kibinafsi kujitolea kuweka na kufanikisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko haya kuanzia mwaka ujao,” inasema taarifa ya COG.
Kaunti ya Makueni inatarajia kuwa miti milioni mbili itapandwa wakati wa kongamano hilo la siku tatu kama njia moja ya kuboresha mazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhutubia kongamano hilo ni Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Wake William Ruto na Spika wa Seneti Ken Lusaka.