Habari Mseto

Koome akosoa Ruto kwa kushambulia mahakama

Na  KEVIN CHERUIYOT November 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JAJI Mkuu Martha Koome ametetea uhuru wa mahakama kufuatia kauli za hivi majuzi za Rais William Ruto akishutumu baadhi ya maamuzi dhidi ya serikali yake.

Jaji Mkuu alisema shutuma hizo hazina msingi wowote akisisitiza kuwa Mahakama ita sheria kila wakati licha ya kushambuliwa na wakuu wa serikali na wabunge.

“Serikali Kuu au wabunge wanapolalamikia kazi ya mahakama, sisi pia tunalalamikia ubadhirifu wao na tutatetea uhuru wa mahakama kwa nguvu zote. Hii ni kwa sababu kama majaji na mahakimu tunafaa kuamua kesi kwa uhuru,” Jaji Koome alisema.

Rais wa Mahakama ya Juu alizungumza Alhamisi kwenye mahojiano na kituo cha redio cha SpiceFM.

Alisisitiza kuwa mihimili mitatu ya serikali inapaswa kufanya kazi kwa uhuru, na kwamba kujadili masuala ya mahakama katika majukwaa ya umma hakutakuwa suluhu.

“Kama umekerwa na uamuzi wa hakimu, tafadhali usiwatukane kanisani, kwenye mazishi, mikutano ya hadhara kwa sababu hatuna namna ya kujibu, rufaa katika mahakama kuu itarekebisha kosa kama lipo,” alisema.