Korti yafuta dhamana ya mshukiwa wa ubakaji Lang’ata
MAHAKAMA ya Kibera jijini Nairobi imefutilia mbali dhamana iliyotoa kwa mwanaume anayetuhumiwa alimbaka mwanamke eneo la Lang’ata.
Korti ilifikia uamuzi huu baada ya mshukiwa kutoroka kutoka jijini alipoachiliwa kwa dhamana.
Hakimu Mkuu Mkazi William Tulel alibatilisha dhamana aliyopewa Elisha Kipkorir Yego baada upande wa mashtaka kutuma ombi iondolewe.
Hakimu aliambiwa kuwa Bw Yego alitoroka na kukosa kufika kortini alipohitajika.
Tukio hili lililazimisha upande wa mashtaka kutuma ombi la kutaka atiwe mbaroni.
Bw Yego anashukiwa kuhusika na ubakaji wa mwanamke katika mtaa wa Royal Park, Lang’ata mnamo Februari 8, 2022.
Vile vile anakabiliwa na shtaka la kumpapasa mwanamke huyo bila idhini.
Aliachiliwa kwa dhamana na akatoweka.
Wakiomba kufutwa kwa masharti ya bondi, upande wa mashtaka ulisema mshukiwa anaweza kusafiri nje ya nchi hadi ughaibuni.
Polisi walimsaka na kumpata kwao mashinani, Mlango, Kaunti ya Uasin Gishu.
Kulingana na Sheria ya Makosa ya Kingono nchini, mshukiwa wa kosa la ubakaji akipatakina na hatia, hufungwa jela miaka 10, kifungo ambacho kinaweza kuzidishwa kuwa cha maisha gerezani kutegemea uzito wa kesi.
Kesi hiyo itasikilizwa Januari 24, 2025.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan